Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAKAMU wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha uhuru wa Mahakama, ikitambua umuhimu wake katika ujenzi wa Taifa, ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu.
Dkt. Nchimbi alisema hayo alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Tambukareli jijini Dodoma.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.

Alibainisha kuwa juhudi hizo zitatekelezwa hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo katika kata zote nchini ambazo bado hazina mahakama hizo.
Aidha, Makamu wa Rais alisisitiza kuwa uhuru wa Mahakama usitumike kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki.

Alisema uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba na Sheria za nchi.
Aliongeza kuwa Mahakama ina wajibu mkubwa wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.
Dkt. Nchimbi alisema Mahakama ina mchango muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kwa kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba, kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki, kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria, kukuza uwajibikaji na nidhamu katika sekta za umma na binafsi, pamoja na kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Aidha, alisema Mahakama ina wajibu wa kuzuia migogoro inayoweza kusababisha migawanyiko ya kijamii au kisiasa, kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri za kisheria zilizo wazi, kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria na taasisi za umma, kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, pamoja na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuhakikishiwa ulinzi wa haki zao za kisheria.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliwaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi kuheshimu tume iliyoundwa na Rais kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kwa kuacha kuyajadili masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa kufuatia ombi la Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, aliyeomba viongozi kuacha kuzungumzia suala hilo kwa namna inayowaumiza wananchi.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, alisema Mahakama inaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa utendaji.
Alisema Mahakama ipo katika hatua za mwisho za kujenga mfumo unaotumia Akili Unde (AI) kwa ajili ya kurekodi mwenendo wa mashauri na hukumu mahakamani.
Alifafanua kuwa kupitia mfumo huo, Jaji, Hakimu, Wakili na Shahidi wanapozungumza, mfumo utatafsiri na kuandika mazungumzo hayo kwa lugha iliyochaguliwa kwa wakati halisi.
Aliongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yataondoa changamoto za ucheleweshaji na upotoshaji unaoweza kujitokeza wakati wa kuchukua kumbukumbu kwa kuandika kwa mkono au kutumia kompyuta.


