Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imekuwa ikihimiza taasisi za fedha kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati.
Hayo yameelezwa leo Februari 25, 2025 Kahama mkoani Shinyanga na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt. Doto Biteko wakati akizindua tawi la Benki ya Exim katika eneo hilo.
“ Eneo hili ni kitovu kikubwa cha shughuli za kiuchumi, hasa sekta ya madini ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa.
Mbali ya madini, mji huu pia ni maarufu katika sekta ya kilimo na biashara. Ni wazi kuwa ufanisi wa sekta hizi unategemea upatikanaji wa huduma za kifedha imara na zinazokidhi mahitaji ya wajasiriamali na wafanyabiashara,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ametaja manufaa ya kufungua tawi eneo hilo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa fursa za uchumi kwa kuongeza ajira, kuongeza mapato ya benki na hivyo kutumia sehemu ya faida yake kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia makundi maalum kadhaa yenye uhitaj.
Aidha,amesema manufaa mengine ni kuongezeka kwa mapato ya kodi Serikalini na kuongezeka kwa ushindani wa huduma za kibenki.
Pia, Dkt. Biteko ameipongeza benki hiyo kwa hatua kubwa na kwa jitihada zake za kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Comoros, Uganda, Djibouti, pamoja na Ethiopia.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za kifedha na kuhakikisha kuwa zinapatikana kwa urahisi na kwa ufanisi kwa kila Mtanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema kuwa ufunguzi wa tawi la benki hiyo ni kielelezo kuwa shughuli za uchumi ni nyingi na zitaendelea kuimarishwa.
Ameongeza kuwa Mkoa huo una matawi ya benki 11 ambayo yote pia yapo Kahama hivyo ni kiashiria kuwa Kahama ipo kibiashara na kuwa Mkoa huo uko tayari kushirikiana na benki hiyo.
Naye, Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja amesema kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kifedha na kuwa dira iliyopo imekuwa ikiwaongoza na ni mpango mkuu wa sekta ya fedha ulioandaliwa na Serikali umeweka mazingira wezeshi na moja ya manufaa yake ni kufunguliwa kwa tawi hilo la benki.
Pamoja na hayo, amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya watoa huduma wasio waaminifu na mikopo chechefu, hivyo Wizara kupitia Benki Kuu imeendelea kukabiliana na changamoto hizo kwa kutoa elimu ya masuala ya fedha mijini na vijijini ili wananchi waelewe na kutumia fursa za fedha zilizopo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu amesema benki hiyo si tu imesaidia katika sekta ya afya bali hata elimu, ubunifu na kuwezesha wajasiriamali wanawake.