Na Lucy Lyatuu
SERIKALI imesema sekta ya huduma inachangia takribani asilimia 45 ya Pato la Taifa la Tanzania kwa mwaka 2024, ikiongozwa na biashara, uchukuzi, huduma za kifedha, TEHAMA, elimu na utalii.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Sempeho Manongi, amesema hayo leo jijini Dar Es Salaam katika hotuba yake kwenye warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa biashara ambayo imeandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).
Amesema sekta ya huduma ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa wa Tanzania na kichocheo kikuu cha ukuaji na ajira.
Amesema sekta ya utalii pekee iliingiza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 3.3 mwaka 2023, na kuajiri zaidi ya Watanzania milioni 1.5 moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja.
Ameongeza kuwa sekta ya TEHAMA, inayoendeshwa na ubunifu wa kidijitali na muunganisho wa simu, inachangia karibu asilimia mbili ya Pato la Taifa, huku sekta ya huduma za kifedha ikiendelea kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha, na kwa sasa inafikia zaidi ya asilimia 75 ya watu wazima kupitia mifumo ya simu na dijitali.
Manongi amesema mauzo ya huduma za Tanzania nje ya nchi yanakua hasa katika utalii, usafiri, na huduma za kitaaluma sehemu ya mauzo ya huduma katika mauzo ya nje inabaki chini ya asilimia 25, ikilinganishwa na zaidi ya asilimia 40 katika uchumi wa juu.
“Hii inaonyesha wazi uwezo ambao hatujatumika katika kuwaweka watoa huduma wa Tanzania katika ushindani wa kikanda na kimataifa,” amesema na kuongeza kuwa warsha kama hiyo ni muhimu katika kuwawezesha watoa huduma kutoka kwa waendeshaji wa vifaa na wahandisi hadi washauri na makampuni ya ICT – kuelewa mahitaji ya upatikanaji wa soko, mifumo ya udhibiti, na mikakati ya kuuza nje.
Amesema kwa mfano kampuni ya Kitanzania ya ICT yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam hivi karibuni ilishirikiana na kampuni ya Rwanda iliyoanzisha mafunzo ya kielektroniki katika EAC, ikionyesha uwezo wa ushirikiano wa kuvuka mipaka chini ya mifumo ya AfCFTA na EAC.

Vile vile, amesema kampuni ya ushauri ya ndani ya Arusha ilifanikisha zabuni ya EAC kuhusu huduma za maendeleo ya biashara kuonyesha jinsi ujuzi wa kujenga uwezo na kufuata unaweza kutafsiri moja kwa moja katika mafanikio ya mauzo ya nje.
Amesema warsha hiyo itatoa moduli za vitendo kuhusu mikakati ya kuingia sokoni, uzingatiaji wa udhibiti, utoaji zabuni, na kuendeleza mipango ya soko la nje, ambayo yote ni muhimu kwa kufungua fursa za usafirishaji wa huduma.
Ameongeza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata mafanikio makubwa katika kurahisisha biashara ya huduma chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikijumuisha sekta saba za kipaumbele zikiwemo biashara, mawasiliano, usambazaji, elimu, fedha, utalii na huduma za usafiri.

Akizungumza, Ofisa wa Sera na Sheria, Hidaya Mkwizu kutoka EABC akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Adrian Njau amesema warsha hiyo inalenga makampuni yaliyo tayari kuuza nje ya nchi katika sekta za huduma za kipaumbele na itazingatia matumizi ya vitendo ya sheria, kanuni na dhana za biashara ili kuongeza ushiriki katika biashara ya kikanda na bara.
Amesema nchini Tanzania sekta ya huduma inaendelea kupanuka kwa kasi, huku kukiwa na ufanisi mkubwa katika sekta ya utalii, usafiri, usafirishaji, TEHAMA, fedha na elimu.

Kaimu Mtendaji wa Shirikisho La Wafanyabiashara Tanzania (TPSF) Deogratius Masawe, amesema warsha hiyo ni kwa ajili ya mafunzo ambapo wafanyabiashara watafundishwa namna ya kufanya biashara nje ya Tanzania wafundishwe mbinu na kujadili changamoto.