Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini ameyataka Mashirika yanayojihusisha na vijana kuwatengenezea mfumo wenye tija na msaada kwa taifa katika umri mdogo kwa lengo la kukuza chachu ya maendeleo.
Sagini amezungumza hayo wakati wa maadhimisho ya Kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Sheikh Kaluta Amir Abeid, na miaka 60 ya kifo chake iliyofanyika Dar es Salaam.
Amesema Kaluta alifanya mapinduzi ya kimaendeleo akiwa na umri mdogo zaidi kushika nyadhifa mbalimbali kuhakikisha anacha alama ambayo ni kumbukizi kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Naibu Waziri amemwelezea Kaluta kwamba alikuwa na mchango katika kukuza kiswahili, kuhakikisha kinaenea kupitia kitabu cha kanuni za ushairi na Kitabu cha Diwani ya Amri.
“Nitahakikisha Wizara ya Katiba na sheria tunaandaa Sheria kwa Lugha ya Kiswahili ili kuwaenzi Waasisi waliopigania Lugha hii inafika duniani kote,bali pia Kurahisisha Mawasiliano baina ya watu ambao hawawezi kutumia lugha ya Kiingereza ambapo kwa sasa watu wengi wanapitia kadhia ya kusoma mikataba na sheria kwa Lugha ambayo kwao imekuwa changamoto. ” amesema.
Sagini ametoa wito pia kwa Baraza la Kiswahili Taifa (BAKITA ) na Wadau Wengine wa Lugha ya Kiswahili kuendeleza kuandaa Makongamano ambayo Kimsingi ina lengo la kukuza lugha ya Kiswahili .
Pia ametoa rai Kwa Vijana kujifunza kutoa mchango kwa taifa huku akizikumbusha taasisi zinazohihusisha na Vijana kuweka mifumo rafiki ili waweze kuwaandaa Vijana na Kuwawezesha Kulitumikia taifa mapema .
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo Hamis Mwinjuma amesisitiza umuhimu wa tukio la Kuwaenzi Mashujaa , akieleza kuwa linaangazia mchango wa Sheikh Kaluta Amri Abeid katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, hasa katika nyanja za sarufi, fasihi, na utangazaji wa Kiswahili duniani.
“‘Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza Kiswahili, ikiwa ni pamoja na kuenzi kazi za mashujaa kama Sheikh Kaluta, na kuhakikisha lugha hii inazidi kuwa nyenzo ya maendeleo na utambulisho wetu kama Taifa.'” amesema.
Naye Mwakilishi Taasisi ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Amiri Abeid Kaluta ametoa Pongezi kwa Viongozi, Taasisi,Makampuni na Mashirika ambayo yamefanikisha Kumbukizi hiyo .