Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Wataalam wa Rasilimali Watu na Utawala Tanzania (THRAPA), kimeandaa Mkutano wa wataalaam kutoka sekta mbalimbali nchini, kujadili na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma mahala pa kazi kulingana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
Mwenyekiti wa THRAPA, Christopher Mwansasu amesema hayo Mkoani Dar es Salaam leo, Mei 13, 2025 alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mkutano huo utakaofanyia katika Hoteli ya New Amaan Visiwani Zanzibar, kuanzia Mei 20 hadi 22 mwaka huu 2023.
Mwansasu amesema mkutano huo utaambatana na maadhimisho ya siku ya Rasilimali Watu Duniani na Mkutano Mkuu wa Mwaka.
Ametaja kauli mbiu ya siku hiyo ni, ‘Uwezo wa Nguvukazi ya Baadaye, Inayoendeshwa na Akili Bandia’.
Amesema Mgeni Rasmi atakuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ally Mwinyi.
“Njoo tujifunze teknolojia mpya za kitaaluma na viwango vya ubora mahala pa kazi. Tukuze taaluma na kujenga mtandao wa kitaaluma,” amesema.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Denis Derua amesema kuwa changamoto za taaluma zinasababishwa na mazingira kulingaa na nyakati.
“Hata changamoto za ajira namna ya kusimamia watu. Kwa kuwa tunapambana kuona namna gani tunashauri watu, tunashauri mwajiri, tunaishauri serikali na tumekuwa sehemu ya kushirikiana na serikali,” amesema.
Kwa upande wake mjumbe wa chama hicho, Bruno Daniel amesema kitaalam kuna mazingira ya kazi yanahitaji uzoefu wa utendaji.
Amewataka waajiri kuchukua wanafunzi na kuwajengea uzoefu.
“Rai yetu ni kuwahamasisha wanachama kukumbusha waajiri wawe na mipango thabiti kufundisha ili wawe na uwezo wa kuajirika,” amesema.
Pia amesema wana taasisi ya kutoa mafunzo na mitihani ya ithibati, pia watakuwa na mafunzo kuhakikisha wataalamu wao wanapikwa vizuri.