Na Lucy Ngowi
CHAMA cha Wafanyakazi wa Taasisi na Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari, Ufundi Stadi na Utafiti (RAAWU),
kimeelezea baadhi ya mafanikio yake hasa katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano na sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kurudishwa kazini watumishi wa darasa la saba walioondolewa kazini kimakosa, wakiwepo wafanyakazi 177 kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kilichopo Morogoro.
Katibu wa Elimu RAAWU, Baraka Shekimweri ameishukuru serikali kwa namna inavyoshughulikia madai mbalimbali ya wafanyakazi katika sekta za RAAWU, japo amesema yapo baadhi ya mambo kama uidhinishwaji mikataba ya halibora yapo katika hatua za ufuatiliaji.
Shekimweri ambaye amezungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu RAAWU, Joseph Sayo amesema pia chama hicho kimepigania malipo ya malimbikizo ya mishahara ya wasaidizi wa wana taaluma kutoka vyuo Vikuu vya umma,
Ambapo hadi sasa madai kwa baashi ya wanufaika kutoka Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) na SUA wameshalipwa fedha zao na wengine bado wapo kwenye foleni.
Katika hilo RAAWU inaendelea na ufuatiliaji madai hayo ili wahusika au familia zao kwa wale walio staafu au kufariki waweze kulipwa.
Mbali na hilo, amesema chama hicho kwa kushirikiana na TUCTA kimepigania kulipwa michango ya watumishi waliokuwa na vyeti feki ikiwa ni pamoja na kuwaombea wasishtakiwe kwa jinai kutokana na udanganyifu na uhujumu uchumi.
Jambo lingine ameeleza kuwa chama hicho kimeshiriki katika majadiliano na serikali pamoja na mfuko wa Bima ya Afya kuongezwa kwa umri wa wategemezi kutoka umri wa miaka 18 hadi 21.
Vile vile RAAWU imeshiriki katika majadiliano yaliyosababisha kuondolewa kwa tozo ya ongezeko la thamani yaani kwa wanufaika wa bodi ya mikopo ambayo ilizalisha madeni makubwa kwa wanufaika hayo yaliyokuwa hayalipiki.