Na Danson Kaijage
DODOMA: WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa programu maalum ya uendelezaji upya maeneo yaliyochakaa katika miji mbalimbali nchini ili kutatua migogoro ya ardhi.
Waziri wa wizara hiyo, Deogratius Ndejembi amesema hayo alipokuwa akisoma taarifa ya Maendeleo ya Wizara yake kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO Jijini Dodoma
Ndejembi amesema, programu hiyo itasaidia kuboresha huduma za msingi katika maeneo hayo na hivyo kuyawezesha kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.
“Programu hii imelenga kuboresha maisha ya wakazi, kupunguza umaskini, kuongeza fursa za kiuchumi na kuhakikisha miji inakuwa endelevu na inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa na majengo, miundombinu na huduma bora zaidi kwa Watanzania.
“Kupitia Programu hii, jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.349 yameainishwa katika mikoa 24 kwa ajili ya kupangwa na kuendelezwa upya ili kuwa na tija kiuchumi na kijamii.
“Kwa sasa wizara ina mpango wa kuboresha maeneo chakavu ya Makangira kata ya Msasani, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni; Maanga Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Unga Limited Halmashauri ya Jiji la Arusha; na Igogo Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
” Hivyo, nitoe wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika kufanikisha utekelezaji wa programu hii ili kuleta mapinduzi yatakayobadilisha mandhari na taswira za miji yetu,” amesema.
Pia amesema serikali imekamilisha marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na hivyo kuwa na Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 (Toleo la mwaka 2023) na tayari imezinduliwa tarehe 17 Machi 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Malengo makuu ya Sera hiyo ni kuhakikisha kuna mfumo madhubuti wa umiliki wa ardhi, usawa katika upatikanaji ardhi, usimamizi na matumizi ya ardhi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Pia amesema, Wizara imepokea Sh. Bilioni 64.5 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika Halmashauri 131 ikiwemo Sh. Bilioni 50 zilizokopeshwa kwenye Halmashauri 57 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi.
Fedha hizo zimewezesha upangaji na upimaji wa viwanja 556,191.
Pia amesema Wizara imetekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.
Kwamba Mradi huo umewezesha uhakiki wa mipaka ya vijiji 871 na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 846 katika halmashauri 21 pia jumla ya vipande vya ardhi 583,734 vimehakikiwa na vimepandishwa katika mfumo wa e-Ardhi.
Amesema hati za Hakimiliki za Kimila 318,868 zimesajiliwa katika vijiji 236 vya wilaya sita za Songwe, Chamwino, Mufindi, Mbinga, Maswa na Tanganyika.
Mradi huo pia umewezesha urasimishaji wa makazi 136,129 katika Halmashauri za Jiji la Dodoma; Wilaya za Chalinze na Songea; Manispaa za Kahama, Shinyanga, Kigoma na Mtwara; na Mji wa Nzega.