Na Lucy Ngowi
Katika dunia inayokabiliana na changamoto za ongezeko la watu, mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa ardhi ya kilimo, jina la Profesa Joseph Ndunguru limeendelea kung’aa katika giza la wasiwasi wa mustakabali wa chakula.
Profesa Ndunguru kwa miaka mingi, amekuwa mstari wa mbele katika tafiti za kilimo, uvumbuzi wa teknolojia, na uongozi unaoleta matumaini mapya katika sekta ya kilimo si nchini Tanzania pekee, bali duniani.

Akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Ndunguru amejijengea taswira ya mtaalamu makini, mtafiti mwenye maono na kiongozi anayegusa maisha ya wakulima wadogo, vijana na wanawake makundi yanayobeba uzalishaji wa chakula barani Afrika.
Safari ya Mawazo Iliyozaa Kitabu cha Kimataifa
Katika mahojiano maalumu, Profesa Ndunguru anaeleza kwa utulivu kilichomsukuma kuandika kitabu chake kipya, ‘ Mageuzi ya Kilimo Duniani, Safari ya Utoshelevu wa Chakula, Uendelevu na Teknolojia’
Kinachoonekana kama kitabu ni zaidi ya maneno ni mkusanyiko wa fikra za miaka, tafiti, uzoefu wa kitaaluma na tathmini ya kina kuhusu hali ya kilimo ulimwenguni.
Anasema kitabu hicho kinajaribu kujibu swali moja muhimu ambalo dunia nzima imeendelea kujiuliza:
“Ni kwa namna gani tutajihakikishia chakula cha watu zaidi ya bilioni 10 bila kuiumiza sayari yetu?”
Swali hilo limekuwa dira yake katika safari ya utafiti na uongozi, na ndilo linaloongoza sura zote 17 za kitabu ambacho kimechapishwa na Visionaly Publishers ya Marekani na karibuni kitapatikana kwenye majukwaa ya kimataifa kama Amazon.

Mtafiti Mwenye Macho Mawili La Sayansi na La Jamii
Tofauti na wataalamu wengi wanaotazama kilimo kama kazi ya kuzalisha tu, Profesa Ndunguru anatizama kilimo kama mfumo mpana wenye vipande vingi vinavyohusiana: ardhi, mazingira, teknolojia, sera, siasa za kimataifa, na utu wa mkulima.
Ndani ya kitabu hiki anachambua historia ya kilimo tangu binadamu walipoanza kulima zaidi ya miaka 12,000 iliyopita hadi mapinduzi ya viwanda na teknolojia ya karne ya 21. Kisha anapendekeza majawabu ya kisasa kama matumizi ya teknolojia za umwagiliaji, mbegu bora, ufuatiliaji wa tabianchi, mifumo ya taarifa za kilimo, na kilimo makini kinachotumia takwimu.

Lakini Profesa Ndunguru haishi tu kwenye maabara; anatambua kuwa kilimo ni maisha ya watu. Ndiyo maana anasisitiza umuhimu wa sera thabiti zisizopinduliwa kila siku, uwekezaji wa kutosha kutoka serikalini na sekta binafsi, na ushirikishwaji wa makundi yote muhimu hususan wanawake, vijana na wakulima wadogo.
Msisitizo wa Makundi Yaliyosahaulika Katika kitabu hiki, sura maalumu zimeandikwa kwa ajili ya: Vijana: Takribani bilioni 1.2 duniani wao ndiyo nguvu kazi ya kesho. Profesa Ndunguru anaelezea vikwazo vinavyowazuia kuingia kwenye kilimo na namna teknolojia mpya zinavyoweza kuwavutia.
Wanawake: Licha ya kuwa uti wa mgongo wa uzalishaji, bado wanakabiliwa na changamoto za umiliki wa ardhi, mitaji na maamuzi. Anasisitiza kuwa mageuzi yoyote yatakayowaacha nyuma hayawezi kuwa endelevu.
Wakulima wadogo: Hawa ndiye injini ya kilimo cha Tanzania, wakifikia asilimia 70–80 ya wakulima wote. Profesa Ndunguru anaweka wazi kuwa bila kuwainua wao, hakuna mageuzi yoyote yatakayoshika mizizi.
Kushindana na Karne Ijayo
Moja ya sehemu zenye mvuto mkubwa katika kitabu chake ni sura inayotazama kilimo cha miaka 100 ijayo. Hapa Profesa Ndunguru anaelezea kwa ufasaha jinsi akili bandia (AI), roboti, kompyuta zenye nguvu ya juu, mifumo ya kuchambua udongo na utabiri wa tabianchi vitakavyobadilisha sura ya kilimo.
Huu ni mwelekeo unaodhihirisha kwamba macho ya Profesa Ndunguru yako mbele ya wakati, na anaiandikia dunia “ramani” ya teknolojia itakayoliongoza kilimo katika karne zijazo.
Kitabu Kwa Dunia – Katika Lugha 10
Utafiti huu mkubwa umevuka mipaka ya Tanzania. Tayari kitabu kinatafsiriwa katika lugha 10 ikiwemo Kiswahili na Kifaransa ili kiwafikie wasomaji wengi duniani. Ni ishara nyingine kuwa mawazo yake yanathaminiwa kimataifa.
Profesa Ndunguru anaeleza kuwa uzinduzi wa kitabu hicho utafanywa hivi karibuni baada ya kuthibitishwa na mgeni rasmi.
Kwa macho ya wengi, Profesa Ndunguru ni mkurugenzi. Kwa wataalamu, ni mtafiti wa mfano. Kwa wakulima, ni sauti ya matumaini. Na kwa dunia inayotafuta majibu ya mustakabali wa chakula, yeye ni miongoni mwa wasomi wachache wanaoandika majibu hayo.
Kupitia kitabu chake kipya, ameweka wazi ukweli mmoja:
Mageuzi ya kilimo yanahitaji akili, sayansi, ubunifu, sera thabiti na mioyo inayojali mustakabali wa binadamu.
Profesa Ndunguru ni mmoja wa watu wachache wanaoibeba mioyo hiyo.

