Na Mwandishi Wetu
WANAFUNZI wamekuwa na muitikio mzuri wa kujifunza lugha ya kichina kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi ya China na Tanzania.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Bagamoyo Pwani, Zaitun Shikwazi amesema hayo kwenye kusherehekea maadhimisho ya miaka 20 ya Taasisi ya Confucius, katika Shule ya Sekondari Baobab.
Amesema China ina mahusiano mazuri ya kibiashara lakini kwenye upande wa elimu kuna ushirikiano mzuri na watoto ndio maana wanapenda kujifunza lugha hiyo.
Amesema uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili unaleta matokeo chanya kwenye nyanja ya elimu.
Naye Mkurugenzi Mtanzania Taasisi ya Confucius Profesa Aldin Mutembei, amesema walifarijika kusikia Rais Samia Suluhu Hassan aliposema inatakiwa kuwepo na Shule za mchepuo wa lugha ya kichina.
“Ni muhimu sana kwa watanzania kujifunza lugha ya kichina kwani inasaidia kufungua fursa nyingi za kibiashara lakini pia kupanua ufahamu kwani kwenye lugha saba kubwa duniani na kichina ipo,” amesema.