Na Lucy Ngowi
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola limeimarisha usalama na ulinzi katika mechi za timu za Simba na Yanga zinazotarajiwa kuchezwa kesho Oktoba 19, 2024.
Kamanda wa Jeshi hilo, Jumanne Muliro amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake leo, Oktoba 18, 2024.
Muliro amesema ulinzi huo unaimarishwa kwa sababu kunatarajiwa kuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu zaidi ya 60,000 uwanjani, utakaohusisha wapenzi wa soka wa hapa nchini na nje ya nchi wa timu mbili maarufu za Simba na Yanga.
“Ulinzi utakuwa wa hali ya juu wakati wa mchezo lakini pia baada ya mchezo,” amesema.
Pia amewakumbusha wapenzi wa soka kutokwenda kwenye mchezo huo wakiwa na silaha ya aina yoyote, isipokuwa askari wachache watakaokuwa wamepangwa kazi maalum za kiusalama.
“Askari wachache narudia kipengele hicho hata kama ni askari kama hujapangwa kazi maalum kwenye uwanja ule halafu ukaja na silaha au mamlaka nyingine yoyote hautaruhusiwa,” amesema.
Muliro amesisitiza suala la usalama na upekuzi wa kuingia uwanjani hapo, utapewa kipaumbele kabla ya mchezo, wakati wa mchezo na baada ya mchezo.
“Tumeimarisha mifumo ya usafiri ya kwenda kwenye uwanja ule ipo barabara ambayo tutaifunga kwa muda kwa ajili ya kurahisisha watu kuingia na kutoka kwenye uwanja ule,” amesema.
Amewakumbusha wapenzi wa soka wanaotarajiwa kwenda uwanjani na magari wawe na kadi ya kuingilia na sio vinginevyo.
“Na tusingependa tuwe na mgogoro au mabishano yasiyokuwa na sababu kwa mtu yeyote ambaye anakuja na gari na kutaka kuingia ndani ya uwanja kama hana kadi, tusingependa kulaumiana katika kipengele kile,” amesema.
Kwa upande mwingine amependa kuwakumbusha wapenzi wa soka wawe na tiketi zao mapema ili waweze kuingia mapema kuepusha msongamano wa watu ambao baadaye wanakuwa ni sehemu ya kusababisha fujo wakati wa kuingia uwanjani.
Amewataka wapenda soka na wanamichezo kuendelea kuwa wastarabu, kujiepusha na vitendo vya aibu.
“Jeshi la polisi linawakumbusha mashabiki wa soka kuendelea kuwa wastaarabu, washangilie kwa ustarabu na kujiepusha na vitendo vya aibu kabla, wakati wa mchezo au baada ya mchezo,” amesema.
Amesema jeshi hilo linawatakia kila la heri timu zote na kuzikumbusha matokeo yoyote yatakayotokea wayakubali.
“Jeshi la polisi linakumbusha timu hizi na mashabiki wake kuyakubali matokeo yoyote yatakayotokea kwa sababu mara kadha tumekumbushwa mchezo wa soka una matokeo matatu kutoka sare, kushinda au kushindwa na kwa kanuni hiyo lazima moja kati ya hayo matatu litatokea kesho Oktoba 19, 2024,” amesema.