Na Mwandishi Wetu
WATUMISHI wa Serikali za Mitaa wamepatiwa mafunzo ya Ufuatiliaji naTathmini ili kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi inayowekezwa na serikali.
Mafunzo hayo yametolewa na Chuo
Kikuu Huria Tanzania (OUT), kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI.
Kaimu Mkurugenzi kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Mussa Otieno amesema hayo alipomwakilisha Katibu Mkuu Adolf Ndunguru, wakati akifungua mafunzo ya awamu ya pili ya Ufuatiliaji na Tathmini

Amesema mafunzo hayo yanafanyika ili kuwaimarisha watumishi waliopo katika idara hizo kwani wataimarika katika utendaji wao wa kazi.
“Baada ya mafunzo haya mtumishi atakuwa na uwezo wa kutimiza malengo yanayotakiwa katika masuala ya ufuatiliaji na tathmini ili miradi ya serikali iendane na malengo yaliyopangwa.
“Tukatumie vyema utaalam tutaopata hapa na tukawashirikishe na wenzetu tunaofanya nao kazi pamoja, ili kuwa na timu nzuri kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika halmashauri tunazotoka,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini wa Utendaji wa serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu amesema serikali za mitaa ndiyo mtekelezaji mkubwa wa shughuli za serikali karibia asilimia 70 ya shughuli zote zinatekelezwa na mamlaka ya serikali za mitaa.
Mratibu wa Mafunzo ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka OUT, Dkt. Emmanuel Mallya amesema chuo hicho kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, kinaendesha mafunzo hayo ili serikali iweze kushuhudia mabadiliko makubwa ambayo yanalenga kuimarisha utendajikazi hasa katika upande wa ufuatiliaji na tathmini.
Mwenyekiti wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Katibu Tawala msaidizi sehemu ya Usimamizi, Ufutiliaji na Ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Pius Ngaiza, ameishukuru serikali kwa kuwapa mafunzo hayo kwa kuwa wengi walikuwa wanafanya tathmini na ufuatiliaji katika namna ambayo ilileta shida hasa katika ukaguzi,.
Amesema mafunzo hayo yamewaimarisha hivyo watafanya kazi kwa kufuata mfumo unaotakiwa kiofisi na hata kitaifa.