Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu Huria cha Tanzania ( OUT), kimesaini mkataba wa ujenzi wa maabara tatu na Mkandarasi Arm Strong Int. Ltd, ambao utakuwa ni wa miezi nane.
Makamu Mkuu wa OUT Profesa Elifas Bisanda amesema hayo katika hafla ya utiaji saini huo iliyofanyika Makao Makuu ya chuo hicho Jijini Dar es Salaam.
Profesa Bisanda amesema mkataba huo uliosainiwa wa ujenzi wa maabara hizo upo chini ya chuo hicho kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ( HEET).

Amesema mradi wa HEET hauwezi kuwa wa maana kama vitafanyika vitu ambavyo havitaleta mabadiliko katika jamii.
“Uwepo wa mradi huu ni sehemu ya maeneo saba ya utekelezaji wa HEET. Tunalenga kujenga maabara za kisayansi, tunatambua nchi haiwezi kuendelea au kubadilika bila kuweka msisitizo kwenye sayansi,” amesema.
Amesema mkandarasa waliyeingia naye mkataba atajenga maabara tatu katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Kigoma. Maabara nyingine zilizobakia zitajengwa na wakandarasi tofauti tofauti.
Naibu Makamu Mkuu wa OUT upande wa Taaluma, Tafiti na Huduma za ushauri. Profesa Alex Makulilo amesema mradi huo unaotekelezwa na chuo hicho kwa thamani ya dola milioni tisa.
Amesema fedha hizo zimegawanyika katika vipengele mbalimbali , kwani asilimia 75 ya mradi mzima zinaenda kwenye ujenzi, maabara saba katika Kanda saba.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Arm Strong Int. Ltd, Pastory Masota amesema wakandarasi ni watekelezaji wa mradi ukiooitia michakato mingi, kupitiwa na watu wengi.
Amesema wao wataweka yote waliyokubaliana katika hali halisi.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Joseph Kuzilwa amesema kuna uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji wa elimu na ukuaji wa uchumi.