Na Lucy Ngowi
HIVI karibuni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), wamefanya semina kwa waandishi wanachama wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), kwa ajili ya kuwapa elimu na uelewa wawapo katika maeneo yao ya kazi.
Miongoni mwa mada zilizofundishwa kwa waandishi hao ni pamoja na Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na 5 ya Mwaka 2003 na kanuni zake.
Wakili wa Osha Rehema Msekwa anaeleza hayo katika semina hiyo iliyofanyika Mkoani Dar es Salaam ambayo iliwakutanisha waandishi wa mkoa huo na wa Pwani.
Anaeleza kuwa lengo la kutekeleza sheria ni kuweka viwango vya usimamizi wa afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi wawapo kazini.
Pia kuondoa ama kupunguza mazingira hatarishi ya kazi, kuweka adhabu kwa waajiri na wamiliki wa maeneo ya kazi wanaokiuka sheria.
Sheria ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ina Sehemu 10 ikiwemo ya utawala katika utekelezaji wa sheria.
“Sehemu hii inaelezea uteuzi wa Mkaguzi Mkuu pamoja na mamlaka aliyopewa kufanya uteuzi wa wakaguzi kwa ajili ya utekelezaji wa sheria.
“Pia imetoa utaratibu wa kila mwajiri kuteua wawakilishi na kuunda kamati za Usalama na Afya kwenye maeneo yao ya kazi,” anasema.
Maelezo yake ni kwamba, sheria hiyo inatoa mamlaka kwa wakaguzi kufanya uchunguzi wa ajali iliyotokea Mahali Pa Kazi.
Na inampa haki mwenye eneo la kazi kukata rufaa kwa Mkaguzi Mkuu kama atakuwa hajaridhika na uamuzi wa Mkaguzi kwa Mkaguzi.
Akielezea usajili wa sehemu za kazi, anasema hilo ni eneo ambapo linaelekeza kusajiliwa kwa maeneo yote ya kazi pamoja na matakwa ya maeneo ya kazi kuwa na leseni ya ithibati baada ya kukidhi viwango vya Usalama na Afya.
Vile vile sheria inaelekeza kuwasilishwa kwa michoro ya majengo kwa mkaguzi mkuu.
Kuhusu masharti ya usalama, anasema waajiri wanapaswa kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa afya pale wanapoingia kazini, wanapoendelea kuwa kazini na wanapofika ukomo wa ajira.
Katika eneo la afya na hali bora maeneo ya kazi, sheria inaelekeza waajiri kuwapatia wafanyakazi maji safi na salama ya kunywa.
Pia inaelekeza uwepo wa vyoo kwa kuzingatia mahitaji ya jinsia na makundi maalumu, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa sanduku ama vifaa vya huduma ya kwanza.
“Sanduku hili litakuwa chini ya usimamizi wa mtu aliyepata mafunzo ya huduma ya kwanza,” anasema.
Jambo lingine ni kuzingatia masharti maalum ya usalama kwa kufanya tathmini za athari za kiusalama na afya katika maeneo ya kazi.
Kuwapatia wafanyakazi vifaa kinga pamoja na usalama na afya katika shughuli za kilimo.
Katika eneo lingine wakili huyo anasema uwekwaji wa umeme katika sehemu za kazi lazima uzingatie maelekezo ya kitaalamu. Vile vile tahadhari ichukuliwe juu ya matumizi ya kemikali hatarishi.
Pamoja na tahadhari ya kufanyakazi maeneo yenye mionzi hatarishi.
Katika eneo la matumizi ya kemikali anasema kuwepo na alama za tahadhari katika kila kifungashio cha kemikali, kuwepo na maelekezo ambapo mfanyakazi atadhurika na kemikali, na mtu yoyote atakeyevunja sheria hiyo, kanuni au amri atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa sheria
Kwamba ikibainika kutenda kosa hilo atalipa faini au kifungo au vyote viwili.
Wakili Msekwa anaelezea wajibu wa mfanyakazi kuwa ni kuzingatia kanuni zinazolinda usalama na afya yake kazini, kutumia vifaa kinga anavyopewa vya kulinda afya na usalama wake kazini.
Vile vile kutofanya mambo ambayo yanaweza kuhatarisha afya na usalama wake au wa wafanyakazi wengine eneo la kazi.
Kuhusu wajibu wa mwajiri, Msekwa anasema ni kuhakikish kadri itakavyowezekana, afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi kazini na urekebu wa wafanyakazi waliopata madhara.
Pia kufanya matengenezo ya mashine na mitambo ili iwe salama kuondoa athari za kiafya, kuhakikisha usalama na kutokuwepo kwa athari za afya katika shughuli za uzalishaji, Usindikaji, matumizi, utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa vitu hatarishi.
Pia kutoa maelekezo, mafunzo na usimamizi ili kuhakikisha afya na usalama wa wafanyakazi wake.
Akielezea namna ya kukidhi matakwa ya sheria ni pamoja na kuwa na kisanduku cha huduma ya kwanza pamoja na mtoa huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha eneo la kazi linafanyiwa na OSHA kaguzi zote zinazostahili kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma anasema chama kitatamani wanachama wake wapate mafunzo ya kutosha, hivyo mafunzo hayo yatakuwa chachu katika maeneo ya kazi kwa waandishi wa habari.
“Lazima tufanye mafunzo kwa wanahabari kuwafundisha vihatarishi, kama JOWUTA tunakagua tuone waandishi wanafanya kazi katika mazingira gani,” anasema.
Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA,Suleiman Msuya amesema chama hicho kinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na hivi sasa kina jumla ya wanachama 400 nchi nzima.
Anaona OSHA iendelee kutoa mafunzo hayo kwa wanachama wengine waliopo mikoani.