– TARI Yatangaza Mbegu 22 Mpya Za Kisasa
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NYANYA aina ya cheri zile ndogo ndogo tamu zenye rangi nyekundu na virutubisho vingi, ambazo zilipotea kwenye soko kwa muda mrefu, sasa zimerejea baada ya kufanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Mtafiti Mwandamizi kutoka Kituo cha TARI Tengeru, Emmanuel Laswai amesema Kituo hicho kinachojihusisha na utafiti wa mazao ya mbogamboga, matunda, viungo na vikolezo, kimefika na mbegu mpya aina 22, katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba mkoani Dar es Salaam.
Amesema mbegu hizo zinalenga kuboresha uzalishaji wa mazao na kukidhi mahitaji ya wakulima pamoja na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Laswai amesema mbegu hizo mpya ni matokeo ya kazi ya miaka kadhaa ya utafiti, zikilenga kustahimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi, magonjwa, na kuongeza tija.
“Katika nyanya, tumezalisha aina sita mpya, mojawapo ikiwa nyanya ya cheri ile ndogo iliyokuwa imepotea kwa muda mrefu.
“Tumeboresha mbegu hiyo, sasa ina mavuno mengi, haishambuliwi sana na magonjwa, na inawavutia watumiaji hususan kwenye hoteli na migahawa ya kisasa jijini Arusha na Dar es Salaam,” amesema.

Amesema pia wana aina mpya za pilipili hoho za rangi nyekundu na ya njano ambazo sasa zinaweza kulimwa nje ya kitalu nyumba, tofauti na ilivyozoeleka.
“Aina mpya za pilipili aina ya abanero maarufu kwa ladha na harufu yake zimeboreshwa kwa uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa ya virusi na bakteria, na kuleta chaguo la rangi mbalimbali kama njano, machungwa na nyekundu,,” amesema.

Amesema pia wametafiti ngogwe chungu iambayo ni mboga maarufu ya asili ilikuwa imeadimika sokoni.
Laswai anasema wamezalisha aina tatu mpya za ngogwe, mojawapo ikiwa ile ya muundo wa mshumaa, maarufu sokoni, lakini sasa ikiwa na ladha ya uchungu zaidi kama ilivyokuwa asili yake.
“Hii ngogwe chungu ni mahsusi kwa wale waliokuwa wanaikumbuka na kuhitaji ladha ya asili. Tuliboresha lakini hatukuondoa uchungu wake ambao ndio sifa kuu ya nyanyachungu,” amesema.

TARI Tengeru inawaalika wakulima na wadau wote wa kilimo cha mbogamboga kujipatia mbegu hizo mpya kwa lengo la kuongeza tija, ubora wa bidhaa, na kuongeza kipato kupitia kilimo cha kisasa chenye tija.
