Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAKALA wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) umefungua milango kwa wadau mbalimbali kushiriki katika biashara ya nafaka, kwa kuwataka wafanyabiashara, wakulima na wananchi kununua nafaka zilizohifadhiwa kwa ubora ili ziuzwe katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwenye Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba, Ofisa Masoko wa NFRA, Eva Michael amesema wakala upo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa chakula,
Ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wafanyabiashara na wakulima kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa thamani wa uhifadhi wa chakula nchini.
“Tupo hapa kutoa elimu ya uhifadhi wa chakula, lakini pia kuwakaribisha wadau wote wanaotaka kushiriki kwenye biashara ya nafaka. Kwa sasa tunaendelea na maandalizi ya awali ya msimu wa ununuzi wa nafaka mpya, lakini pia tunaendelea na mauzo ya nafaka zilizopo,” amesema.
Amesema NFRA ina akiba ya kutosha ya nafaka katika maghala yake, ikiwa ni pamoja na mahindi, mpunga, mtama mweupe, mbaazi na dengu, huku akisisitiza kuwa chakula hicho ni salama na kimetunzwa kwa viwango vya kitaalamu.
Amebainisha kuwa fursa hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara wanaotaka kupata nafaka kwa bei nafuu na kuuza kwenye masoko mbalimbali, hatua inayolenga pia kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo na biashara.
Wakala wa NFRA ni taasisi ya serikali inayoshughulika na uhifadhi wa chakula cha dharura kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya njaa, lakini pia imekuwa mshirika muhimu wa sekta binafsi kupitia usambazaji wa nafaka kwa ajili ya biashara.