Na Danson Kaijage,
DODOMA: BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema limejipanga kuhakikisha linavuna magugu maji mapya katika ziwa Victoria.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Sware Semesi alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassani kwa Waandishi wa Habari katika ukumbi wa wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dodoma.
Amesema NEMC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira pamoja na nchi jirani zinazopakana na Ziwa Victoria, wamefanya juhudi kuokoa ziwa hilo kutokana na kuibuka magugu maji mapya ambayo yanaweza kusababisha changamoto mbalimbali katika ziwa hilo.
Amesema kama magugu maji hayatavunwa yataitesa miundombinu katika ziwa hilo, kusababisha vivuko kuingiliwa maji na kukwamishaji uwekezaji unaofanywa katika ziwa hilo.
Pia amesema kwa miaka minne ya 2020/21 hadi 2024/25, baraza hilo limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia zaidi ya asilimia 68 ya malengo yaliyowekwa.
“Katika utekelezaji wa Miradi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) baraza limesajili jumla ya miradi 8,058, kati ya hiyo 5,784 ni ya TAM na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira.
“Vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio ya taarifa za TAM na Ukaguzi wa Miradi na kutoa mapendekezo ya maboresho ya masuala ya msingi ya kuzingatiwa katika taarifa hizo. Miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira.
“Kati ya hivyo, 3,058 ni vya TAM, 765 ni vya Ukaguzi, huku vyeti vingine vikiwemo vya kubadili masharti 169, vyeti vilivyohamishwa umiliki 552, vyeti vya muda (PEC) 53 na cheti kilichorudishwa,” amesema.
Ameeleza kuwa Kabla ya mfumo Baraza lilikuwa linasajili takribani miradi 900 kwa mwaka na baada ya mfumo Baraza linasajili zaidi ya miradi 2,000 kwa mwaka, jambo ambalo aliawma ni mageuzi makubwa ya Serikali ya awamu ya Sita.
“Vilevile, kaguzi zilifanyika katika maeneo 178 ya uzalishaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki, ambapo maeneo 57 yalikutwa na makosa na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.
“Zaidi ya Tani 150 za vifungashio visivyokidhi viwango vilikamatwa, vikataifishwa na kuteketezwa kwa mujibu wa Sheria,” amesema.