Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MTAKWIMU Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Boniface Simpoli, amesema takwimu si kwa ajili ya wataalamu peke yao, bali ni nyenzo muhimu kwa kila mwananchi, wakiwemo wafanyabiashara wadogo.

Amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hii katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
“Takwimu ni mwanga. Ukishakuwa na huo mwanga, hata mama ntilie anaweza kupanga vizuri biashara yake na kuikuza,” anasema Simpoli.
Kwa mujibu wa Simpoli, NBS huzalisha takwimu rasmi katika makundi matatu makuu ya kijamii, kiuchumi na mazingira.

Amesema takwimu hizo zina taarifa muhimu zinazoweza kumsaidia mama ntilie kupanga kwa ufanisi, kufuatilia mwenendo wa soko, na kujua wapi kuna fursa zaidi za biashara.
Takwimu za kijamii, kama zile zilizotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zinaweza kutoa mwanga kwa mama ntilie kuhusu wapi afanye huduma zake.
“Kwa mfano, akijua kuwa mtaa fulani una idadi kubwa ya wanaume ambao hawajaoa, anaweza kufungua mgahawa wake hapo kwa sababu kuna uwezekano mkubwa kuwa hawapiki nyumbani. Hiyo ni fursa ya soko,” amesema.
Amesema takwimu hizo pia zinaonyesha idadi ya watu kwa jinsi, hali ya ndoa, na makadirio ya ongezeko la watu hadi mwaka 2050, taarifa ambazo ni muhimu kwa mfanyabiashara kupanga maendeleo ya muda mrefu.
Amesema mbali na takwimu za kijamii, mama ntilie anaweza kufaidika na takwimu za kiuchumi, hasa katika kilimo. Kwa mfano, kwa kujua mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mazao kama viazi, nyanya au maharage, anaweza kupanga manunuzi ya chakula kwa bei nafuu moja kwa moja kutoka mashambani, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.
“Ukijua wapi kuna uzalishaji mkubwa, na wapi kuna masoko yenye watu wengi, unaweza kupanga safari zako za manunuzi na usambazaji kwa faida zaidi,” amesema.
Kwa mfano, takwimu zinaweza kuonyesha kuwa Mkoa wa Iringa una uzalishaji mkubwa wa nyanya, huku Dar es Salaam ikiwa na soko kubwa la bidhaa hiyo. Mama ntilie anaweza kutumia taarifa hiyo kupanga biashara ya nyanya kwa ufanisi mkubwa.
Amesena Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia takwimu katika maisha ya kila siku.
“Mama ntilie asione kama takwimu ni za maofisini tu. Ziko kwa ajili yake pia. Akizielewa, anaweza kufanya maamuzi bora zaidi, kupunguza hasara, na kuongeza kipato,” amesema.