Na Mwandishi Wetu
LINDI: MGOMBEA urais wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema yuko tayari kushirikiana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa endapo atapewa ridhaa na Watanzania katika uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka huu 2025.

Akizungumza na wananchi wa Ruangwa mkoani Lindi, Mwalim amesema hawezi kumdharau Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuwa amelitumikia taifa kwa miaka 10.
“Nitakapokuwa Rais nitafanya naye kazi Mzee Majaliwa. Nitalinda heshima na maslahi yake kama Waziri Mkuu. Huyu mzee atakuwa mshauri wangu, hata katika safari za nje nitamwomba twende pamoja maana ana uzoefu mkubwa,” amesema Mwalim.
Aidha, Mwalim ameahidi kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kulingana na mazingira ya kazi zao.
“Angalieni polisi wetu wanavyofanya kazi vizuri. Tangu nimeanza kampeni nawapongeza kwa ushirikiano mzuri,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali ya CHAUMMA itashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama bila kufanya mabadiliko ya haraka katika uongozi.
“Sina IGP mwingine, ma-RPC, DC wengine—nitafanya kazi nao hawa hawa. Wanafanya vizuri tutawapongeza, wakikosea tutawakosoa,” amesema.
Mwalim amewataka wananchi wa Ruangwa kuwachagua viongozi watakaowatetea, si kwa misingi ya vyama.
“Msiende kuchagua chama, chagueni mtu atakayesema shida zenu. Nani amewahi kuona Mzee Majaliwa akivaa nguo za chama bungeni? Ndani ya Bunge hakuna mwenyekiti wa chama, hakuna katibu mkuu, bali wabunge wanaowakilisha wananchi wao.
“Msisubiri tena ‘iyena iyena, tieni tieni’ mkidhani chama kitawaletea barabara au bei nzuri ya korosho. Chagueni watu watakaowapigania kweli,” ameseama

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Ruangwa kupitia CHAUMMA, Njalila Ally, amesema pamoja na changamoto za kiuchumi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya mambo mengi mazuri ya kukumbukwa.
“Waziri Mkuu Majaliwa amefanya kazi kubwa na tutamkumbuka, ikiwemo kuanzisha timu ya Namungo,” amesema Njalila.