Na Mwandishi Wetu
SIMIYU: MGOMBEA urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amewataka wananchi wa Maswa Mashariki kumchagua mlezi na mwalimu wake wa siasa, John Shibuda, kuwa mbunge wao.
Akizungumza katika mkutano wa lala salama wa kampeni, Mwalim amesema Shibuda ni mwanasiasa mkongwe ambaye akienda bungeni ataweza kuzisemea changamoto na shida za Wasukuma.
“Oktoba 29 hebu twendeni na mlezi na mwalimu wa siasa aliyenilea kwa muda mrefu… huyu sina shaka naye kabisa. Mzee Shibuda ni nguli wa siasa na wazee kama hawa ni wachache,” amesema.
Mwalim amewataka WanaMaswa kuzingatia kauli ya Baba wa Taifa, Mwalim Julius Nyerere, ya mwaka 1962 kwamba hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo.
Aidha, amesema atarejesha heshima ya Wasukuma ya kuamini kuwa jembe ni utajiri.
“Jembe ni utajiri, kwani likilima pamba, watoto watasoma na wanaume wataoa wanawake zaidi ya mmoja.
“Hamwezi kutatua matatizo yenu kwa kukubali vitu vidogovidogo kama mabango, kofia, tisheti. Nendeni mkaikatae CCM,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwalim amewataka Waislamu kuwachagua viongozi wanaofaa ili waweze kulisaidia taifa, alipotoa wito huo baada ya kuswali Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Marampaka, Simiyu.

