Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KATIKA jitihada za kuinua viwango vya maadili kwenye tafiti za kibinadamu na utoaji wa huduma za afya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Ndaki ya Insia, Idara ya Falsafa na Stadi za Kidini, kimefanya mradi unaolenga kuimarisha misingi ya maadili katika sekta ya afya nchini Tanzania.
UDSM imefanya mradi huo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oslo (Norway) na Chuo Kikuu cha Rwanda.
Mtafiti kutoka UDSM, Shija Kuhumba amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Habari katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema mradi huo umejikita katika kutathmini, kuboresha na kusambaza mbinu bora za maadili zinazoweza kutumiwa na wataalamu wa afya, watafiti na watunga sera nchini.
Kwa mujibu wa Shija mradi huo ulikuwa na kazi kuu nne ambazo ni Utafiti Kuhusu Maadili Katika Sekta ya Afya ambapo timu ya watafiti ilifanya mahojiano na madaktari, manesi na wakuu wa hospitali katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ili kuchunguza changamoto za maadili katika mazingira halisi ya kazi.
Amesema pia wametengeneza Kozi ya Mafunzo ya Maadili iliyoandaliwa kwa ajili ya manesi.
“Kozi hiyo hutumika kama sehemu ya kuhuisha leseni za utabibu, ikiwa ni nyenzo muhimu kwa watoa huduma ili kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kimaadili,” amesema.
Vile vile amesema walitengeneza Kamati ya Maadili ya Tiba yenye jukumu la kushughulikia migogoro ya kimaadili kama mgonjwa anayekataa matibabu kutokana na sababu za kidini au kitamaduni.
Amesema Kamati hiyo pia inatoa ushauri katika utungaji wa sera za afya, ikizingatia kuwa maadili ni nguzo muhimu hasa inapokuja kwenye usawa wa upatikanaji wa huduma, mgawanyo wa rasilimali chache, na heshima ya utu wa binadamu.
“Kamati ya maadili imekuwa msaada mkubwa kwa madaktari wanaokumbwa na changamoto ngumu za kimaadili.
“Wakati mwingine daktari anakumbwa na mtanziko kati ya kutekeleza wajibu wake wa kitabibu na kuheshimu maamuzi ya mgonjwa ambaye kwa sababu za imani au tamaduni anakataa matibabu,” amesema.
Pia amesema, “Katika mazingira yenye uhaba wa vifaa tiba, uamuzi wa nani aanze kupata huduma ni suala la kimaadili pia. Mradi huu umetengeneza miongozo ya kusaidia watoa huduma kufanya maamuzi magumu kwa kuzingatia haki, usawa na utu wa mgonjwa,”.
Mradi umetoa mapendekezo kwa serikali kuhakikisha kwamba sera ya afya kwa wote inaendana na hali halisi inayowakabili watoa huduma. Ulisisitiza kuwa afya si suala la kibaiolojia tu, bali linagusa jamii nzima, ikiwemo mila, dini na mitazamo ya kijamii.