KATIKA Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka jana 2024, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), lilitoa hoja zake kwa serikali miongoni mwa hoja hizo ilikuwa ni kuiwezesha Tume Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kuweza kufanya kazi zake kwa uweledi.
Hoja hizo zilitolewa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda mbele ya Makamu wa Rais,Dkt. Philip Mpango ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Habari njema ni kwamba, serikali imeweza kutekeleza hoja hizo ambazo zilitolewa siku ya wafanyakazi mwaka jana.
Mkurugenzi Mkuu CMA, Usekelege Mpulla anasema kwamba serikali imejibu hoja za TUCTA kwa kuongeza watumishi, kuboresha huduma zake kwa kuzisogeza karibu na wananchi pamoja na vitendea kazi.
Kuhusu kuongezewa watumishi anasema kwamba, serikali imewaongezea watumishi 11 kati ya hao wasuluhishi ni wanne, mwamuzi mmoja, waandishi wa ofisi wawili, ugavi mmoja, watunza kumbukumbu wawili na mkaguzi wa ndani mmoja.
“Ni kweli mwaka jana TUCTA ilitoa hoja tatu kwa serikali kuhusu CMA na zote zimetekelezwa. Hadi tunavyozungumza watumishi wameongezwa, wasuluhishi, waamuzi, wakaguzi, ugavi na kada nyingine. Serikali imeongeza watumishi kama ilivyoombwa,” anasema.
Anaongeza kuwa kupitia Mradi serikali iliipa tume fedha za kuendesha mradi wa usimamizi wa migogoro kidijitali, na kwamba kupitia mradi huo mambo makubwa mawili yamefanyika.
Mpulla anataja mambo hayo kuwa ni kujenga miundombinu ya TEHAMA katika ofisi 32 za tume mikoa yote, pili kununua vitendea kazi zikiwemo kompyuta. “ Serikali imewezesha hilo,”.
Anasema, “Mkakati wa serikali kusogeza huduma kwa wananchi itawezesha walio mbali kusajili kesi zao pasipo kusafiri kufuata ofisi zilipo,”.
Maelezo ya Mkurugenzi ni kwamba, mradi huu utaanza kutumika rasmi mwaka mpya wa fedha Julai mosi, 2025.
“Serikali imetekeleza yale maombi ya TUCTA. Kimsingi itaendelea kutekeleza. Pia ina mkakati wa kuiwezesha tume kuboresha huduma kupitia tume inayotembea. “Hilo pia linaendelea kufanyiwa kazi,”.
Anasema mradi huo umegharimu Sh. Bilioni 2.1, pia serikali imeongeza zaidi ya Sh. Milioni 900 bajeti ya mwaka 24\25.
Mkurungenzi Mkuu huyo anasema hayo ni miongoni mwa hoja ambazo ziliwasilishwa kwa serikali Mei Mosi mwaka jana 2024.
Akiwasilisha hoja hizo kwa Makamu wa Rais Dkt. Mpango, Katibu Mkuu TUCTA, Mkunda alieleza kuwa migogoro ya kikazi inatakiwa itatuliwe kwa weledi na haraka ili wahusika waendelee kuzalisha na kutoa huduma kwa maendeleo ya Taifa.
Anasema utaratibu uliopo kwa Watumishi wa Umma wa kushughulikia Migogoro ya Kikazi kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002, kupitia Tume ya Utumishi wa Umma ni mrefu sana,
Na unatumia muda mrefu kiasi kwamba Wafanyakazi wengine wanafuatilia mashauri yao hadi muda wa kustaafu kazi unafika kabla hawajapata haki zao.
HivyoTUCTA inashauri utaratibu uliokuwa unatumika kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini sura ya 366 rekebisho la mwaka 2019 kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na ikibidi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi utumike kwa Wafanyakazi wa Sekta zote yaani Sekta ya Umma na Binafsi.
Naye Dkt. Mpango kwenye maadhimisho ya mwaka jana, alisema kuwa Serikali imepokea pia ushauri kuhusu kuiongezea CMA watumishi na vitendea kazi ili kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za CMA kwa kuipatia vitendea kazi ikiwemo magari na kuongeza idadi ya watumishi kulingana na uwezo wa kibajeti.
“Mfano, kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 Serikali ilitoa kibali kwa Tume cha kuajiri watumishi nane, mwaka 2022/23 watumishi 16 na 2024/25 nafasi 24 zimetengwa kwa ajili ya ajira mpya.
Aidha, Serikali inaendelea kusimika Mifumo ya Kielektroniki ya usajili, utatuzi na usimamizi wa migogoro ya kazi. Mifumo hii itawezesha Wafanyakazi na Waajiri popote walipo kusajili migogoro ya kazi ikiwemo kutumia simu-janja pasipo kulazimika kuzifuata Ofisi za CMA.