Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAA: TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeandaa kambi maalum ya uchunguzi na ushauri wa kitabibu kwa wazee, itakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kuanzia kesho Oktoba 16 hadi 18, mwaka huu 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi, huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya kibingwa na kibobezi katika maeneo ya mifupa, ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu, pamoja na huduma za mazoezi tiba na ushauri wa tiba lishe.
Mvungi ameeleza kambi hiyo imelenga kuboresha afya za wazee na kuwapatia nafasi ya kupata huduma za kitaalamu kwa urahisi.
Amesema huduma hizo zitakuwa bure kwa wazee wasio na bima ya afya, huku wenye bima wakitumia bima zao kama kawaida.
Aidha, MOI imewahimiza wazee wote kujitokeza kwa wingi katika kambi hiyo ili kuchangamkia fursa hii muhimu ya kuboresha afya zao.