Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa na unafuu katika upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ili kumwezesha kila mwananchi kutumia nishati iliyo safi na salama.
Biteko amesema hayo Septemba 13, 2024 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa nishati safi ya Kupikia yenye thamani ya Sh. Bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Jeshi la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia.
Hafla hiyo imeenda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yanayowezesha sekta ya nishati kuendeshwa kwa mafanikio kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuokoa maisha ya watanzania.

“Pia kuiwezesha Wizara ya Nishati kutatua changamoto zinazojitokeza lengo likiwa ni kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi,” amesema.
Kuhusu usambazaji nishati vijijini ikiwemo umeme, Biteko ameipongeza Bodi na Menejimenti ya REA kwa kusimamia ipasavyo miradi kwa kuwahimiza wakandarasi kukamilisha kazi kwa wakati.
Kwa upande wa jengo lililozinduliwa la ghorofa tano lenye thamani ya Sh. Bilioni 9.8, Biteko amesema litawawezesha watumishi kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema tukio hilo ni alama ya ushirikiano kati ya REA na Taasisi za Jeshi.
Ameishukuru serikali kwa jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti wa rasilimali za misitu na kutengeneza fursa za ajira kupitia Nishati Safi ya Kupikia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameishukuru serikali kwa kutoa Sh. Bilioni 214 kwa ajili ya shughuli za umeme mijini na vijijini ambapo mkoani Dodoma asilimia 92.2 ya vijiji vimefikiwa na umeme huku kazi hiyo usambazaji umeme ikiendelea.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia alilolitoa wakati akizindua mjadala wa kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia.
Na kutilia mkazo wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia hivyo Wizara ya Nishati ina wajibu wa kutekeleza agizo hilo, ndio maana taasisi yake ya REA imesaini mikataba
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Saidy amesema Wakala kuhamia kwenye jengo lake kumewezesha kuokoa Sh. Milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo ya huduma zinazotolewa na Wakala.
Saidy amesema kwa upande wa JKT mikataba iliyosainiwa ina thamani ya Shilingii Bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 76 ambayo ni sawa na Sh. Bilioni 4.37 itatolewa na REA na huku asilimia 24 sawa na Sh. Bilioni 1.39 itatolewa na JKT.