Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA urais kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, Ambary Haji Khamis, amewataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika mikutano ya kampeni iliyofanyika jimboni Ilemela, jijini Mwanza, Khamis amesema kuwa ni jukumu la kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, kwa kuwa ni haki yao ya kikatiba na kisheria.
“Twendeni tukapige kura Watanzania wenzangu… twendeni, vijana, wakina mama na wazee tukaichague NCCR-Mageuzi,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa chama hicho, Dk. Eveline Munisi, amewataka wananchi kudumisha amani na utulivu wakati wote wa kipindi cha uchaguzi ili kuwezesha ushiriki mpana na salama wa wapiga kura.
Dk. Munisi amesisitiza Tanzania imeendelea kuwa kimbilio la amani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, tofauti na mataifa mengine yanayokumbwa na migogoro.
“Endapo amani hiyo itavunjika, Watanzania hawatakuwa na pa kukimbilia,” alionya Dk. Munisi.
Chama cha NCCR-Mageuzi ni miongoni mwa vyama vinavyowania nafasi ya juu ya uongozi nchini katika uchaguzi mkuu ujao. Kampeni zinaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi huku vyama na wagombea wakihimiza ushiriki wa kidemokrasia na utulivu wa kisiasa.