Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, amesema atajenga Soko la Kisasa la Kimataifa katika eneo la Feri.
Akizungumza na wafanyabiashara na wachuuzi wa soko la Kivukoni, amesema kuwa pamoja na kujenga soko hilo, ataweka utaratibu wa ruzuku ili waweze kuendesha vizuri biashara zao.

“Tutajenga soko jipya la kimataifa… lakini tutaanza kuboresha soko ili kwanza hakuna kinachoshindikana. Ninaomba mtuamini,” amesema.
Aidha, amesema atajenga viwanda vya uchakataji wa minofu ya samaki ili vijana waweze kupata ajira.
Amewataka wananchi kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu na siyo kususia. Mwalim aliwataka kupiga kura ya ukombozi kwa kukichagua CHAUMMA, akisema kuwa CCM haina huruma na Watanzania.

“Najua hapa siongei na wachuuzi wa samaki peke yao, wote mnajua kuwa changamoto ni nyingi sana jijini Dar es Salaam… sasa twendeni tukapige kura ya ukombozi,” amesisitiza.
Naye mgombea nafasi ya Makamu wa Rais kupitia CHAUMMA, Debotha Minja, aliwataka wananchi kufanya maamuzi ya kukichagua chama hicho ili ushuru wa soko la samaki utekeleze wajibu wake ipasavyo.