Na Lucy Ngowi
MBUNGE wa Viti Maalum, Christina Mndeme, amesema kuna umuhimu wa kuongeza wigo wa upatikanaji wa majiko ya gesi na majiko banifu kwa ruzuku, akipongeza taasisi 1,136 ambazo zimeitikia wito wa kutumia nishati safi ya kupikia kwa vitendo.
Amesema hayo hayo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mipango ya utekelezaji ya Dira ya Taifa 2050.
Amesema bado zipo taasisi ambazo hazijaunga mkono juhudi hizo, hivyo ameshauri kuwekwa kwa sheria, kanuni na miongozo itakayozisimamia taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ili zilazimike kutumia nishati safi ya kupikia.
Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi yasibaki kuwa ya hiari, bali yawe ya lazima kwa mujibu wa sheria na taratibu, kwa lengo la kulinda mazingira.
Christina ameongeza kuwa kwa sasa kaya takribani 2,000 zinatumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia, hivyo ameshauri kuongezwa kwa wigo wa matumizi ya gesi asilia majumbani.
Ameeleza kuwa ajenda ya nishati safi ya kupikia, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeleta mafanikio makubwa ambapo idadi ya watumiaji wa nishati safi imeongezeka kutoka asilimia 6.9 hadi 23.2 kwa sasa.
Katika hilo, amempongeza Rais Samia kwa kutoa ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi 452,445 ya gesi ya kilo 6, pamoja na ruzuku ya asilimia 85 kwa majiko banifu 200,000 yaliyotolewa kwa wananchi waishio vijijini, ambapo wanufaika wakubwa ni wanawake.
Amesisitiza kuwa nishati safi ya kupikia ni uchumi, ni afya na ni mazingira, na kuomba kuendelezwa kwa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi kama ilivyoelekezwa katika Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa na Rais Mei 2024.
Christina pia ameshauri kuwepo kwa uwekezaji zaidi katika nishati safi ya kupikia, kupunguzwa kwa tozo na kodi kwenye nishati safi, teknolojia zake pamoja na mashine za kutengeneza majiko, ili viweze kupatikana kwa bei nafuu.
Aidha, amependekeza matumizi ya teknolojia ya ‘pay as you use’, ambapo mtumiaji hulipa kulingana na kiwango cha matumizi ya gesi.’
Kwa ujumla, amesisitiza kuwekwa kwa mazingira rafiki yatakayowezesha wawekezaji kuwekeza zaidi katika sekta ya nishati safi ya kupikia, kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kuhimiza matumizi ya nishati safi nchini.

