Na Lucy Ngowi
IRINGA: WAFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga, mkoani Iringa, wanatarajia kukuza uchumi wao kupitia uzalishaji wa maziwa yaliyo bora na salama, baada ya kupatiwa elimu ya kitaalamu kuhusu usafi, uhifadhi na usindikaji wake.
Elimu hiyo imetolewa mkoani Iringa, na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kuhusu afya ya mifugo, hususani ugonjwa wa homa ya kiwele, pamoja na athari za usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

Katika mafunzo hayo, wafugaji wameelekezwa namna sahihi ya kuzalisha maziwa salama na yenye kukidhi viwango vya ubora, jambo ambalo litaongeza kipato, kupanua masoko, ikiwa ni pamoja na kubadili maisha ya familia nyingi.
Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake baada ya mafunzo, Uneiy Chaula kutoka Mafinga amesema elimu waliyoipata imewaongezea maarifa ya kufuga kwa tija na kibiashara.
“Sasa tunaweza kutambua ugonjwa wa kiwele mapema, kutumia vifaa sahihi kama California Mastitis Test (CMT), na kutengeneza bidhaa kama mtindi.

Hii ni fursa ya kuongeza kipato chetu na kuvutia wateja zaidi,” amesema Oscar Ngimba, mfugaji kutoka Mafinga.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye pia ni Mtafiti wa Mradi wa NANO COM, Dkt. Nuria Majaliwa, amesema maziwa ni rasilimali ya thamani yenye mchango mkubwa katika lishe na uchumi wa mfugaji.

Amesema mchango huu unaweza kuonekana kikamilifu endapo tu maziwa hayo yatazalishwa, na kuhifadhiwa kwa kuzingatia kanuni bora za uzalishaji na usalama wa chakula.
Amesema kwa kufanya hivyo maziwa yatakuwa salama kwa mlaji, kukidhi viwango vya ubora vinavyotambulika kitaifa na kimataifa, hivyo kufungua fursa zaidi za kibiashara kwa wafugaji na wajasiriamali wa bidhaa za maziwa.
“Maziwa yanaweza kuwa chanzo cha lishe bora au chanzo cha maradhi endapo hayatazalishwa, kuhifadhiwa na kusindikwa kwa viwango vinavyokubalika. Elimu hii inalenga kuongeza thamani ya maziwa na kukuza kipato,” amesema.
Nqye Daktari wa wanyama wa Halmashauri ya Halmashauri ya wilaya ya Mufind,
Innocent Nguluma amesema elimu hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wafugaji kutambua mbinu bora za usindikaji, usafi wa mazingira na namna bora ya kuzuia magonjwa ya mifugo ambayo huathiri moja kwa moja uzalishaji wa maziwa.
“Kujua namna ya kudhibiti ugonjwa wa kiwele na kutunza maziwa kwa usafi kunafanya uzalishaji wa bidhaa bora sokoni, kipato zaidi kwa mfugaji, na afya bora kwa mlaji,” amesema

Mradi wa NANO COM unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambao unafadhiliwa na Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Utafiti cha Canada (IDRC), unalenga kuimarisha usalama wa chakula, lishe na kipato cha wafugaji kupitia mnyororo wa thamani wa maziwa