Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kuwa makaa ya mawe yana nafasi ya kimkakati katika kuharakisha mageuzi ya uchumi wa Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda.
Ameeleza kuwa rasilimali hiyo si tu chanzo cha nishati, bali pia ni mhimili muhimu katika kuongeza thamani ya madini na malighafi nyingine za viwandani.
Akizungumza Machi 30, 2026 katika kikao na wadau wa makaa ya mawe kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, Mavunde amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya makaa ya mawe yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje,
Kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta mbalimbali, zikiwemo nishati, viwanda na madini.

Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wadau wa sekta hiyo ili kuhakikisha inakua kwa kasi na ufanisi zaidi.
“Makaa ya mawe ni mhimili muhimu katika maendeleo ya viwanda. Tunahitaji kuongeza uzalishaji na kuhakikisha matumizi yake yanaongeza thamani ndani ya nchi,” amesema Mavunde.

Katika kikao hicho, Waziri amepokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara, zikiwemo gharama za uzalishaji, usafirishaji na upatikanaji wa masoko.
Ameahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi changamoto hizo kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Aidha, amesisitiza kuwa upangaji wa bei elekezi utafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wote ili kulinda maslahi ya sekta.

Wadau wa makaa ya mawe waliipongeza Serikali kwa kuwashirikisha katika majadiliano, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza uwazi na imani katika uendeshaji wa sekta.
Wameahidi kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuongeza mapato ya Taifa.
Kwa upande mwingine, Mavunde amewahimiza wadau kuanzisha chama kitakachowaunganisha ili kurahisisha uratibu wa shughuli zao na kushughulikia changamoto kwa pamoja.

Katika kuimarisha viwanda vya ndani, amesema Kampuni ya A1 Steels Tanzania Ltd inapanga kujenga kiwanda cha chuma Dodoma, kitakachotumia takribani tani 20,000 za makaa ya mawe kwa mwaka.
Mradi huo unatarajiwa kuchochea ajira, kuongeza thamani ya madini na kuimarisha uchumi wa Taifa.

