APRILI 5,2024: Kikokotoo cha mafao moto bungeni
SAKATA la kikokotoo cha mafao kwa wastaafu, limeibuka tena bungeni huku Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya, akisema bado ni janga.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba serikali kukaa meza moja na wadau ili kujadili namna bora ya kuwapa mafao yao kutoka asilimia 33 iliyopo sasa hadi 50 kwa mafao ya mkupuo.
Hayo yalijiri alipokuwa akichangia Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2024/25 bungeni.
MEI MOSI, 2024:Matarajio nyongeza mshahara, kikokotoo
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limesema matarajio ya wafanyakazi leo ni nyongeza ya mshahara ambao wanaamini ukiboreshwa vizuri mfanyakazi anapostaafu atapata mafao mazuri.
Kikubwa pia kinachosubiriwa ni kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu.
MEI 26, 2024: TALGWU ‘ yamshukia’ vikali RC Makonda
CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa nchini(TALGWU), kimemtaka mkuu mkoa wa Arusha,Paul Makonda,kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma pale anapozungumza na watumishi wa Umma na kuacha kutoa maneno ya kashfa na dhihaka kwa mtumishi iwe mbele ya hadhara au pasipo hadhara.
Kauli ya TALGWU inakuja baada ya video fupi ikimuonesha Makonda akiwa kwenye mkutano wa hadhara huku akimhoji mtumishi wa Umma katika ziara yake wilayani Longido Mkoani Arusha ambapo katika Video hiyo alionekana akitoa matamshi kwa mtumishi huyo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa Kimataifa (TALGWU),Shani Kibwasali aliagiza hayo alipozungumza na waandishi wa Habari.
JUNI 24, 2024: TUCTA yataka usawa mifuko PSSSF, NSSF kikokotoo
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limeishauri serikali kuangalia upya na kuweka usawa katika nyongeza ya mkupuo ya kikokotoo kwa watumishi walioguswa na mabadiliko ya Sheria ya Utumishi wa Umma, ili kuwe na usawa wa asilimia 40 na kuondoa tofauti iliyopo.
Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, amesema hayo wakati wa kikao cha dharua cha kamati tendaji ya shirikisho hilo kuhusu Bajeti ya Taifa ya mwaka 2024/25 kilichokutana mkoani hapa.
JULAI 27, 2024: Samia amtwisha zigo Ridhiwani PSSSF,NSSF RAIS Samia Suluhu Hassan, aliwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni huku na kuwatwisha majukumu mazito kwa kumtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, kusimamia vizuri mifuko ya hifadhi ya jamii iwe endelevu na isifilisike.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo Ikulu, Dar es Salaam alipokuwa akiwaapisha mawaziri wawili, Naibu Mawaziri na Makatibu Tawala wa Mikoa miwili.
SEPTEMBA 27, 2024: Masharti watumishi wanandoa kuungana
Serikali yataka orodha ya wanaotaka kuhama kuwafuata wenza wao, yaonya kuhusu udanganyifu.
Dodoma. Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewataka watumishi wa umma wanaotaka kuhama kwa lengo la kuwafuata wenza wao wa ndoa kuwasilisha taarifa kwa waajiri wao kabla au ifikapo Oktoba 5, 2024.
Barua kuhusu wito huo imetolewa na Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Juma Mkomi Septemba 24, 2024 kwenda kwa viongozi wa umma kwa ajili ya utekelezaji.
OKTOBA 16, 2024 Serikali imeonya ukiukwaji wa maadili kwa watumishi wa umma ikiwemo viashiria vya mapenzi ya jinsia moja na mavazi yasiyofaa kwa watumishi wa umma jambo ambalo limekuwa likichafua taswira ya serikali.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Daudi,wakati akifungua kikao kazi cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka simamizi za maadili ya kitaluma
DISEMBA 6, 2024NHIF yarejesha toto afya kadi
TOTO Afya Kadi inarejea. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kuanzia Januari mwakani, watoto wenye umri usiozidi miaka 21 watanufaika nayo.
NHIF ilisitisha Toto Afya Kadi mwaka jana baada ya kubainika ilikuwa inasababisha hasara kubwa kwa mfuko kutokana na kundi hilo kutumia zaidi ya kile ilichokuwa inachangia kwa mfuko.
DISEMBA 30, 2024: Wastaafu 13,000 walipwa mafao kwa kikokotoo kilichoboreshwa
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unaendelea kutekeleza agizo la serikali ulipaji mafao kwa kutumia utaratibu wa kikokotoo kilichoboreshwa.
Uongozi wa mfumo huo umesema kuwa tayari Sh. bilioni 126 zimelipwa kwa wastaafu 13,167 kuanzia Julai Mosi hadi kufikia Desemba mwaka huu.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Yessaya Mwakifulefule alisema hayo wakati wa mafunzo na utoaji elimu kuhusu mfuko huo kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro.
Mwakifulefule alisema mfuko ulianza kulipa mafao kwa wastaafu kuanzia Septemba mwaka huu kwa mujibu wa tamko la serikali lililotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
IMEANDALIWA NA LUCY NGOWI