Na Lucy Ngowi
DODOMA: Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde ametaja thamani ya awali ya mazao tisa yaliyofanyiwa mchakato wa kufungua masoko mapya kuwa ni dola bilioni 3.5 sawa na takribani sh trilioni 10.
Mazao hayo ni parachichi, ndizi, tumbaku, viazi mviringo, vanilla, nanasi, karafuu, pilipili manga na kakao.
Silinde ameeleza hayo alipokuwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Uzinduzi wa Mchakato wa Kufungua Masoko Mapya ya Mazao ya Kipaumbele uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema hiyo ni fursa kila mwananchi anaenda kuichangamkia kwa kufuata vigezo na kutimiza vigezo ambavyo vimewekwa.
“Tunahakikisha kuwa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania ( TPHPA), ndio wenye jukumu la kuhakikisha vile viwango vya nchi nyingine vinafikiwa na wakulima wanapata soko la uhakika katika maeneo yaliyoainishwa,” amesema.
Amesema ili kuhimili ushindani wa masoko ya nje na ufikiwaji wa masoko mapya nje ya nchi inahitajika kutekeleza kikamilifu sheria, taratibu na makato ya usafi wa mimea.
Ametaja nchi hizo kuwa ni China inahitaji vanilla na nanasi, Indonesia karafuu, Singapore karafuu, Israeli parachichi, Malaysia parachichi, Canada pilipili manga.
Nchi nyingine ni Uturuki nanasi, Brazil nanasi, Marekani kakao, Afrika Kusini ndizi, Zambia viazi mviringo, Pakistan tumbaku na Iraki tumbaku.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru amesema hivi karibuni mamlaka hiyo imekamilisha makubaliano baina yake na nchi mbalimbali kwa baadhi ya mazao.
Amesema mamlaka imeanza mchakato wa kupata masoko mapya ya vanilla, kakao, karafuu, pilipili manga, parachichi, ndizi na nanasi kwa msaada kutoka Umoja wa Ulaya na FAO.
“Zaidi ya hayo, kupitia mpango wa serikali wenyewe, pia tutakuwa tunatafuta masoko mapya ya tumbaku,” amesema.