Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa elimu katika juhudi za kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, kwa lengo la kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora katika mazingira salama na rafiki.
Kupitia ushirikiano na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) na kwa ufadhili wa Serikali ya Canada, TEA inatekeleza jumla ya miradi 48 ya ujenzi, ukarabati na umaliziaji wa miundombinu ya elimu katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe.

Atugonza David Ofisa Miradi kutoka TEA akiwa na Mwalimu Maisha Masabile Makamu Mkuu wa shule ya Nyakitonto alipokuwa akikagua hali ya ukarabati wa maabara tatu za Sayansi shuleni hapo.
Ofisa Miradi kutoka TEA, Atugonza David, ameeleza hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo na kuweka vibao vya ufadhili.
Amesema miradi mingi imekamilika na ipo tayari kutumika, huku akisisitiza kuwa maeneo mengi yamelenga ukarabati na uboreshaji wa maabara za sayansi kama sehemu ya kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuongeza ushawishi kwa wanafunzi katika masomo ya sayansi.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakitonto iliyopo Wilayani Kasulu wakifanya mazoezi ya somo la Fizikia kwa vitendo kwenye maabara iliyokarabatiwa na UNICEF, kwa ufadhili wa Serikali ya Canada na kusimamiwa na TEA
Miongoni mwa shule zilizofaidika ni Shule ya Sekondari Nyakitonto, iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma. Shule hiyo ilipokea takriban Sh. Milioni 60 kwa ajili ya ukarabati wa maabara tatu za sayansi.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Maisha Masabile, amesema mradi huo umeleta mageuzi chanya katika ufaulu.

Mwalimu Maisha Masabile Makamu Mkuu wa shule ya Nyakitonto akifafanua jambo kwa Ofisa Miradi kutoka TEA, Atugonza David alipokuwa akikagua hali ya ukarabati wa maabara tatu za Sayansi shuleni hapo.
“Awali tulikosa maabara kabisa na tulikuwa tukifanya mazoezi ya vitendo darasani. Sasa tuna vyumba vitatu vya maabara vilivyokarabatiwa. Mwaka 2024 ufaulu ulikuwa asilimia 100, huku wanafunzi 43 kati ya 150 wakichagua masomo ya sayansi. Mwaka huu 2025, idadi imeongezeka hadi wanafunzi 68 kati ya 210,” amesema Mwalimu Masabile.

Kwa sasa, TEA kwa kushirikiana na UNICEF, inaendelea kutekeleza miradi yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 2.5 katika mikoa hiyo mitatu, kwa lengo la kuinua ubora wa elimu, kuongeza fursa za ujifunzaji na kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora na jumuishi.

Monekano wa kibao cha ufadhili wa maabara tatu za sayansi Shule ya Sekondari Nyakitonto iliyopo Wilayani Kasulu.

Monekano wa jengo la maabara tatu za sayansi zilizofanyiwa ukarabati na UNICEF, kwa ufadhili wa Serikali ya Canada na kusimamiwa na TEA Shule ya Sekondari Nyakitonto iliyopo Wilayani Kasulu.