WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa vyama vya wafanyakazi barani Afrika kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani ili kulinda ajira na kuimarisha ustawi wa wafanyakazi.
Majaliwa ametoa wito huo alipohutubia Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OATUU) uliofanyika mkoani Dar es Salaam, alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesisitiza umuhimu wa mafunzo endelevu kwa wafanyakazi ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo akili mnemba.
“Tunapaswa kuweka mpango wa kutoa mafunzo endelevu yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuwandaa wafanyakazi kwa aina mpya za ajira zinazojitokeza. Teknolojia lazima ilinde utu wa binadamu na si kudhoofisha heshima ya kazi,” amesema.
Amesema mapinduzi ya teknolojia na utandawazi yameleta mabadiliko makubwa katika mazingira ya kazi, na kwamba mitambo na mifumo ya kisasa imeanza kuchukua nafasi ya kazi ambazo hapo awali zilitegemea nguvu kazi ya binadamu.
Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha wafanyakazi wanajengewa uwezo wa kukabiliana na mabadiliko hayo, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia mpya na kulinda haki pamoja na faragha za wafanyakazi.
Amesisitiza kuwa serikali inaendelea kutambua na kuthamini mchango wa vyama vya wafanyakazi katika maendeleo ya taifa, na kwamba uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali na vyama hivyo umechangia maboresho ya sera, sheria na mazingira ya kazi nchini.
“Serikali imevipa nafasi vyama vya wafanyakazi kufanya kazi kwa uhuru na bila kuingiliwa. Tunawasihi kuendelea kushirikiana nasi kwa lengo la kuboresha zaidi maslahi ya wafanyakazi,” amesema.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, amesema serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na vyama vya wafanyakazi kwa kuhakikisha sera na sheria mbalimbali zinarekebishwa ili kulinda haki zao.
Makamu wa Rais wa OATUU, Joshua Ansah, ametoa wito kwa vyama vya wafanyakazi Afrika kuendelea kushikamana katika kutetea usawa na haki za wafanyakazi, huku akiishukuru Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu.
“Tuendelee kuunga mkono Shirikisho letu kwa maslahi mapana ya wafanyakazi barani Afrika. Tukiwa wamoja, tunaweza kusimamia na kupigania haki zao kwa mafanikio zaidi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla, amebainisha kuwa ni muhimu kwa wafanyakazi kuhusishwa moja kwa moja katika kila mabadiliko ya kijamii na teknolojia yanayowahusu.
“Ni lazima wafanyakazi washirikishwe na waandaliwe kwa mabadiliko haya kwa kuwapatia mafunzo stahiki. Mafanikio ya maendeleo haya hayawezi kupatikana bila ustawi wa wafanyakazi,” amesema.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kutetea haki za wafanyakazi nchini yametokana na mahusiano bora kati ya chama hicho na serikali.
“Tumetumia njia ya majadiliano na maridhiano kwa kiasi kikubwa. Serikali yetu imesikiliza changamoto za wafanyakazi na kutafuta suluhisho,” amesema Nyamhokya huku akifurahia Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Afrika (OATUU) lilianzishwa Aprili 1973 kwa juhudi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, kwa lengo la kuunganisha wafanyakazi wa Afrika na kutetea maslahi yao kwa pamoja.