Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekikabidhi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tuzo ya ushindi wa kwanza katika kundi la Elimu ya Juu, Maendeleo ya Ujuzi na Taasisi za Utafiti, kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba.
Majaliwa alikabidhu tuzo hiyo wakati akifunga maonesho hayo jana Julai 13, 2025, yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam.
Tuzo hiyo, iliyotolewa katika hafla ya kufunga maonesho hayo imejumuisha UDSM kama taasisi bora iliyoonesha mchango mkubwa katika kuendeleza ujuzi, maarifa na bunifu kwa maendeleo ya taifa.
Waziri Mkuu Majaliwa, ambaye pia ni mhitimu wa chuo hicho, alilisifu banda la UDSM kwa kuonesha ubunifu unaogusa jamii moja kwa moja, huku akisisitiza umuhimu wa kuunga mkono bidhaa na huduma za ndani.
“Maonesho haya siyo tu jukwaa la biashara, bali ni daraja muhimu la kuunganisha ubunifu, uwekezaji na maendeleo ya viwanda. Tunapaswa kuyachukulia kwa uzito kama mataifa yaliyopiga hatua kama Japan,” amesema. Majaliwa.
Amesisitiza azma ya serikali kujenga uchumi wa ndani unaotegemea uzalishaji wa ndani na maarifa ya Watanzania wenyewe.
“Tunapaswa kuenzi bidhaa, chapa na bunifu zetu za ndani. Taasisi kama UDSM zina nafasi muhimu katika kutimiza azma hii.” amesema.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Utafiti, Profesa Nelson Boniface amesema ushindi huo ni ishara ya mafanikio ya pamoja na wito wa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika suluhisho la changamoto za kitaifa.
“Tuzo hii ni ya kila mwanafunzi, mhadhiri, mtafiti na mshirika aliyeshiriki kutufikisha hapa. Ni ushahidi kwamba tukishirikiana tunaweza kubadili jamii kupitia utafiti na bunifu zenye suluhisho,” amesema.
Banda la UDSM liliwavutia maelfu ya wageni wa ndani na nje kwa ubunifu wa hali ya juu, maonyesho ya kisayansi na teknolojia za kisasa.
Miongoni mwa bunifu zilizosisimua wengi ni kifaa cha kidijitali kinachopima damu bila sindano, kilichobuniwa na mwanafunzi wa kike kutoka Kitivo cha waliotembelea banda hilo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kikwete amepongeza ubunifu na umuhimu wa miradi iliyowasilishwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya UDSM Sabasaba na Mkuu wa Mawasiliano wa UDSM, Dkt. Dotto Kuhenga, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi makini, kazi ya pamoja na kujituma kwa dhati.
“Huu ni ushindi wa kimkakati. UDSM imejipambanua siyo tu kwa kufundisha, bali kwa kubadilisha maarifa kuwa suluhisho linalogusa jamii. Tumejipanga kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya taifa,” amesema.
Ushindi huo unaiimarisha nafasi ya UDSM kama moja ya taasisi zinazoongoza barani Afrika katika elimu ya juu, utafiti na ubunifu. Kwa dhamira ya kulea vipaji, kuendeleza maendeleo jumuishi na kutumia maarifa kubadilisha maisha.