Na Mwandishi Wetu
TANGA: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa juhudi zake katika kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumza leo, Oktoba 16, 2025, alipotembelea banda la mamlaka hiyo kwenye maonesho ya maadhimisho ya Chakula Duniani katika viwanja vya Usagara, Tanga,.
Majaliwa amesema TPHPA imekuwa mfano bora katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu, uhifadhi salama wa mazao na uimarishaji wa usalama wa chakula kuanzia shambani hadi mezani.

Akiipongeza mamlaka hiyo, amesema juhudi zake zimechangia kuhakikisha wakulima, wafanyabiashara na walaji wanazingatia viwango vya ubora na usalama wa chakula, jambo linalolinda afya za Watanzania na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo.
Majaliwa amesisitiza kuwa elimu kuhusu usalama wa chakula ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha vizazi vijavyo vinapata chakula salama na chenye lishe bora.
Maadhimisho hayo ya kitaifa, yaliyoanza Oktoba 10, 2025, yanafikia kilele chake leo yakiongozwa na kaulimbiu “Tuungane Pamoja Kupata Chakula Bora kwa Maisha Bora ya Baadaye.” Kupitia kaulimbiu hiyo, serikali inahimiza ushirikiano wa wadau wote katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama, chenye lishe na endelevu kwa maendeleo ya taifa.