Mwandishi wetu
MONDULI: TAASISI ya Wanahabari ya kusaidia jamii za Asili (MAIPAC) imezindua mpango wa ugawaji bure majiko ya gesi kwa jamii za Asili ili ziweze kutumia nishati safi, salama na kupunguza natumizi ya kuni.

Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fred Lowassa akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma wakikabidhi jiko kwa mwananchi
Mpango huo uliozunduliwa kijiji cha Mbuyuni Monduli jana unalenga kugawa majiko 1000 ikiwa ni jitihada za shirika hilo kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama lakini pia kuunga mkono kampeni ya Rais Samia Suluhu kuhamasisha matumizi ya nishati safi na Salama nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Tasisi ya Smile Youth and Women Support Organization(SYWSO) na kugawa majiko hayo,kijiji cha Mbuyuni wilayani Monduli, Mbunge wa Monduli Fred Lowassa amepongeza MAIPAC na SYWSO kwa kuamua kusaidia jamii.
Katika hafla hiyo iliyohudhuria na mamia ya watu licha ya MAIPAC kutoa majiko, SYWSO na MATT Fondation wamekabidhi baiskeli za wenye ulemavu, fimbo za kutembelea na vifaa vya shule.

Katika hafla hiyo, Lowassa amesema moyo wa kusaidia jamii ambao umeoneshwa na mashirika hayo unafaa kuigwa na wakazi wa Monduli na Watanzania kwa ujumla kwani pia aliyekuwa Mkurugenzi wa IPP Hayati Reginald Mengi alikuwa akifanya hivyo.
Amesema amepata faraja kuona wanahabari wameanzisha taasisi za kusaidia jamii na kuanza na wilaya ya Monduli.
“Mimi binafsi leo nimepata faraja sana kumuona hapa rafiki yangu mwandishi wa habari mahiri Mussa Juma kwani siku nyingi tangu nikiwa kijana mdogo nakumbuka kila siku asubuhi tulikuwa tunasubiri kusoma gazeti la Mwananchi kujua Mussa Juma ameandika nini,” amesema.
Amesema licha ya kuendelea na kazi ya kuandika habari , Juma na wenzake wameamua kuanzisha taasisi za kusaidia jamii hivyo anawapongeza.
Amesema wananchi wa Monduli wamepata faraja kupokea misaada hiyo kwani ni mwendelezo wa misaada inayotolewa na wadau mbalimbali.

Amesena Rais Samia Suluhu Hassan amefanya makubwa katika wilaya hiyo ikiwepo kupeleja mradi mkubwa wa maji wa Sh. Bilioni 27 ambao utasaidia Kata ya Nanja na vijiji 13 vikiwepo vya kata ya Lepurko vya Mbuyuni, Makuyuni na Losimongori.
Amesema pia kilomita tatu za barabara katika kijiji hicho zimeanza kukarabatiwa na kutatua shida ya barabara.
“Lakini pia kutokana na jitihada zangu kama Mbunge niliweza kuonana na Rais Samia kuzungumzia mgogoro wa ardhi ya malisho uliokuwepo hapa Monduli na sasa umetoa uamuzi ardhi hiyo tutatumia kwa pamoja na jeshi letu la wananchi kwa malisho.
“Nawaomba Monduli Oktoba tumpe kura zote Rais Samia kwani ametufanyia mambo makubwa na mengi ikiwepo kutoa fedha sekta za afya, elimu na kusaidia wafugaji,” amesema.
Naye Juma amesema, “Mheshimiwa Mbunge misaada hii inatokana ma michango ya Taasisi za kitanzania na ambazo zimeona umuhimu wa kusaidia jamii badala ya kutegemea mashirika kutoka nje ya nchi na sisi kwa MAIPAC tunaomba wadau waendelee kujitokeza kuchangia majiko ili yasambazwe kwenye.jamii hizi za asili,” amesena.
Amesema Taasisi ya MAIPAC imekuwa na miradi kadhaa wilaya za Longido, Karatu na Monduli ikiwepo Mradi wa ujenzi wa uzio chanzo cha maji cha Kabambe kijiji cha Selela ambao umekamilika .
Amesema mradi huo ni sehemu ya mradi wa kulinda,kuheshimu na kuhifadhi maarifa ya asili ambao unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia programu za miradi midogo inayoratibiwa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa(UNDP) Tanzania na ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira).
Qmesema katika mradi huo MAIPAC hivi karibuni itazindua kitabu cha pili cha maarifa ya asili ya jamii za Asili za Wadzabe, Datoga na Maasai katika uhifadhi wa Mazingira,Vyanzo vya Maji na Misitu.
Ofisa Maendeleo.wa Halmashauri ya wikaya ya Monduli, Fauzia Omar alipongeza shirika la MAIPAC na SYWSO kwa kutoa misaada mbalimbali kwa wilaya hiyo na kutaka waendelee kusaidia jamii.
Ameomba mashirika hayo kufika vijiji vyote 62 katika wilaya hiyo, kushirikiana na serikali kusaidia miradi ya jamii lakini pia kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.