Na Danson Kaijage
DODOMA: WAKAZI wa Jiji la Dodoma wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya usafi wa mara kwa mara katika maeneo yao ya makazi na mahali pa kazi badala ya kusubiri kusukumwa na viongozi.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Afya wa Jiji la Dodoma, John Lugendo,alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Kizota Mtaa wa Relini wakati wa uhamasishaji ufanyaji wa usafi katika kata hiyo.
Lugendo amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi anayeishi katika jiji la Dodoma kufanya usafi katika maeneo yake na kutambua kuwa usafi ni sehemu ya ujenzi wa Afya bora.
“Usafi inatakiwa kuwa sehemu ya tabia ya mwanadamu na usafi ni sehemu ya afya kwani usipokuwa na tabia ya kuwa msafi ni wazi kuwa unaweza kukaribisha magonjwa bila kujua.
“Nil lazima kuzingatia usafi na kuchukia uchafu ikiwa utaendekeza tabia ya uchafu katika sehemu za kazi au kwenye makazi yako hiyo tabia haina tofauti na mtu mwenye tatizo la afya ya akili,” amesema.
Kwa upande wake Sheik wa Kata ya Kizota katika Jiji la Dodoma,Hamed Selemani,ameeleza kuwa suala la usafi ni ibada kamili kwani hata mitume na manabii wote walihimiza usafi.
Kiongozi huyo wa Kiroho ambaye alishiriki suala la usafi amesema ni wajibu wa kila kiumbe kutambua kutokufanya usafi ni sawa na kumtumikia shetani kwani ndiye anayependa mambo ya uchafu kwa maana hata dhambi ni uchafu.