Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “MFUMO wa taarifa kwa abiria unamwezesha anayesubiri abiria, au aliyemsindikiza abiria, kujua mahali basi lake lilipo. Na muda wowote anaweza akafuatilia kwamba lipo wapi,”.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (LATRA), Salum Pazi amesema hayo katika maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema kwa kutumia mfumo huo wa taarifa kwa abiria, mtumiaji anaweza kufungua stendi ya mabasi ambayo yupo.
“Kwa mfano unaweza kufungua niko stendi ya 88 Dodoma, utaonyeshwa mabasi yote yanayowasili au yanayokuja stendi hiyo na yako wapi kwa muda huo na yanatarajiwa kufika hapo saa ngapi.
“Kwa hiyo tunaondoa kabisa ile changamoto ya kusubiri basi haujui litafika saa ngapi au haujui liko wapi, kwa sababu mfumo umerahisisha na unatumia teknolojia ya kisasa ya akili mnembe, kuweza kupiga hesabu ya basi lilipo,” amesema.
Katika hatua nyingine amewakaribisha wadau wa Dar es Salaam na maeneo jirani, kufika katika maonesho hayo kujionea kazi za udhibiti zinavyofanyika.
Ametaja kwa uchache huduma walizonazo kuwa ni kusajili wahudumu wa kwenye mabasi, kufanya usajili wa madereva ambao wanaelekea kufanya mitihani kwa ajilo ya kuthibitishwa.
Pia wanawawezesha watu wanaotuma maombi ya leseni kwa njia ya mtandao.