Na Lucy Ngowi
MOROGORO: UTAFITI uliofanywa jijini Dar es salaam na maeneo mengine ya dunia umeonesha kuwahusisha wanafunzi kwenye shughuli mbalimbali na matukio ya kisayansi kunaongeza uwezo wao wa udadisi na kupenda masomo ya sayansi.
Profesa mbobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Ndaki ya Sayansi asili na Tumizi (CoNAS) Profesa Faith Mabiki amesema hayo wakati akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya ALFAGEMS iliyopo Mkoani Morogoro.
“Tupo hapa leo kwa kuwa tunaamini katika utafiti huo kwamba tunahitaji
kuwashirikisha watoto wetu kwenye matukio ya kisayansi ili kukuza udadisi wao na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ambayo watu huamini kuwa ni magumu,
“Lakini kupitia mafunzo ya aina hii kwa vitendo mara kwa mara na kuipenda kemia wanaweza kuona kuwa masomo ya sayansi sio magumu kama inavyodhaniwa,” amesema.

Amewataka kutambua kuwa nchi inahitaji wakemia wengi ili kusaidia kufanya kazi kwenye viwanda mbalimbali ambavyo Serikali inahamasisha wawekezaji kuja kujenga kwa kuwa bila kufanya hivyo nafasi hizo zitachukuliwa na wageni.
Vile vile amewataka wanafunzi hao na wengine nchini kuona nafasi ya kemia kwenye maisha ya kila siku kwenye kila eneo la maisha akitolea mfano wingi wa bidhaa zinazoongoza kwa kutumiwa madukani zinazotengenezwa kupitia uchanganyaji wa kemikali na kupata bidhaa pendwa kwa jamii ikiwemo vinywaji.

Amesena mafunzo ya iana hiyo yatasaidia kuzalisha idadi ya wanakemia wengi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hayo Mkemia Dkt. Frank Rwegoshora amesema mafunzo ya aina hiyo ni muhimu kwa wanafunzi ambao wana mapenzi na masomo ya kemia,

Ikizingatiwa kuwa ndio wanatarajia kwenda kusoma vyuo vikuu wanahitaji kujua umuhimu na faida za kusoma kemia na fursa zilizopo duniani kupitia fani hiyo muhimu.
“ Kwa kweli tumefurahi sana sisi kama waandaaji lakini pia walimu na zaidi wanafunzi 150 ambao wamejitokeza kwa wingi na kufurahia mafunzo hayo yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo yaliyotolewa na walimu na wabobevu wa kemia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine na tunaamini tumezalisha jeshi la wataalamu wa kemia kupitia mafunzo haya,” amesema.

Dkt. Rwegoshora amesema wamefanikiwa kufikia wanafunzi wa shule hiyo lakini zipo shule nyingi nchini ambazo zina wanafunzi wa aina hiyo na wengine wenye uwezo mkubwa na mapenzi na kusoma kemia na kuwa wakemia,
Lakini wana woga na maneno ya baadhi ya watu kuwa kemia ngumu hivyo wanahitaji kufikiwa na kupewa moyo na kuoneshwa fursa zilizopo ikilinganishwa na masomo mengine.

“Tunatoa shukrani nyingi kwa wafadhili wa mafunzo haya Pan African Chemistry Network na Royal Society of Chemistry kwa msaada wao mkubwa katika kufanikisha hamasa hii muhimu kwa wanafunzi wetu na wanasayansi wachanga,” amesema.
Naye mwanafunzi Maganja Jeremiah amesema wamefurahi kutembelewa na wataalamu hao lakini kubwa zaidi mafunzo hayo yamewaonesha fursa kubwa zilizopo kwenye fani ya kemia pamoja na mchango wa wataalamu wa kemia kwenye maendeleo ya Viwanda na uchumi wa Taifa.
“Tunawashukuru sana hakika binafsi ninasoma mchepuo wa sayansi lakini nilikuwa na woga kuhusu suala la maisha baada ya kuhitimu chuo kikuu fani ya kemia, lakini kwa maelezo na ushahidi uliotolewa na wataalamu hawa kutoka SUA, sina woga tena na nitachagua kusoma SUA fani hii ili niisaidie nchi yangu,” amesema.
Mwanafunzi mwingine Prosper Rey amesema kupitia mafunzo kwa vitendo wamejifunza vitu vingi ambavyo walikuwa hawavifahamu na kuahidi kuendelea kuvitumia kwenye maisha yao ya kila siku.
“Elimu hii itatuwezesha na sisi kuwa mabalozi wazuri wa masomo ya kemia kwa wanafunzi wenzetu na kwa jamii kuondoa woga uliosambaa miongoni mwa watu kuhusu ugumu wa masomo ya sayansi hasa kemia ili jamii zaidi ielewe na kuhamasika kuisoma na kuitumia kwenye maisha yao,” amesema.