Na Mwandishi wetu
ARUSHA: TAASISI ya Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa Arusha (AICC), ) na Taasisi ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wametiliana saini hati ya makubaliano ya Ujenzi wa kituo cha Mikutano Cha kimataifa cha Mlima wa Kilimanjaro kitakachojengwa jijini Arusha.
Aidha ujenzi huo utakamilika ndani ya miaka miwili.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana katika hafla hiyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha za ujenzi wa kituo hicho.
Pia ameagiza wasimamizi wa mradi hu, kuhakikisha ujenzi unaende haraka ili uweze kutumika kwa mkutano mkubwa ikiwemo ule Mkutano wa Dunia wa masuala ya nyuki na asalia mbao unatarajiwa kufanyika nchini, 2027.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo ameishukuru serikali kwa kutoa baraka za ujenzi wa kituo hicho utakao gharimu Sh. Bilioni 385.
Pia ameishukuru taasisi ya PSSSF kwa utayari wake na kutekeleza maelekezo ya mamlaka.
Amesema uwekezaji huo ni mkakati wa Serikali unaolenga kukuza utalii wa mikutano yaani ‘Conference Tourism’.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete amesema ujenzi huo ni maelekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inayoelekeza umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi na muhimu kwa ustawi wa Taifa,
Kiuchumi, kijamii na kiutamaduni pamoja na Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala (CCM) ya mwaka 2021.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Neema Musomba amesema,
“Msajili wa Hazina anapongeza ushirikiano wa PSSSF na AICC, na kuwa ofisi ya Msajili wa Hazina wakati wowote itakuwa tayari kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.”.
Nao watendaji wakuu wa PSSSF na AICC kwa nyakati tofauti wamesisitiza kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha mradi huo kimkakati unakamilika kama ilivyopangwa.