Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “WAPO watu ambao wametoa mchango mkubwa pengine hawajawahi kupata hata diploma, lakini ukiwataja hapa Tanzania kila mtu anajua mchango wake ni wa aina gani,”.
Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabari Tanzania, Mgaya Kingoba, ameeleza hayo alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na Mtangazaji wa Crown Salum Kikeke kuhusu bodi hiyo itamtambuaje mtu mwenye uzoefu ambaye hana elimu ya Diploma ya Uandishi wa Habari na kuendelea.
Amesema sheria inataja watu ambao wametoa mchango kwenye maendeleo ya sekta ya habari Tanzania, kwamba wataangaliwa kwa mujibu wa sheria inavyotamka.
“Kwa sababu kwenye hiyo sheria, Inawataja watangazaji, waandishi wa habari, watayarishaji wa vipindi na wana vyuo wote wametajwa.
‘” Kwa hiyo hatutatoka kwenye ile sheria ya habari kwa kuwa sheria imetuongoza huyo anayeitwa mwandishi wa habari ni nani,” amesema.
Kuhusu leseni kwa mwandishi wa habari amesema inalipiwa Sh. 50,000 kwa miaka miwili, baada ya hapo mwandishi anaomba tena.
“Ipo kwenye mfumo wa kadi inayokuwa rahisi kusomeka kwenye mifumo ya kisasa. Itatolewa badala ya Press Card,” amesema.
Bodi ya Ithibati ya Wanahabari Tanzania imeundwa kwa mujibu wa sheria , lengo kuu ni kukuza taaluma ya waandishi wa habari.