Na Lucy Ngowi
GEITA: MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, amesema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji, na hadi sasa taifa lina akiba ya takribani tani 10 za dhahabu.
Amesema hayo katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Sekta ya Madini, yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, mkoani Geita alipofanya ziara.

Kingalame amesema hatua hiyo ni matokeo ya juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wote.
“BoT imepiga hatua kubwa. Watu wanaendelea kuleta dhahabu na serikali inanunua. Hili linaonyesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi tano bora barani Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali haijawabana wachimbaji, bali imeweka mazingira rafiki yanayowawezesha kuuza dhahabu ndani na hata nje ya mipaka ya Tanzania, kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

“Ni muhimu wachimbaji wa Nyang’hwale na maeneo mengine waelewe kuwa kuuza dhahabu kwa serikali kunasaidia taifa kuwa na akiba ya kutosha. Lakini pia, kila mmoja anafaidika mjasiriamali na taifa kwa ujumla,” amesema.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kufika katika maonesho hayo kujifunza kuhusu teknolojia mbalimbali zinazotumika katika sekta ya madini ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji na uchorongaji wa dhahabu, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta.
Pia amepongeza juhudi za wajasiriamali waliopo kwenye maonesho hayo kwa kuonesha ubunifu na bidii katika kukuza uchumi wa nchi kupitia shughuli zao mbalimbali.
“Wajasiriamali wanafanya kazi kubwa. Nimefurahishwa na namna wanavyojishughulisha na kujipambanua katika utafutaji wa kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu,” amesema.