Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Kilwa Kaskazini Francis Ndulane amewasha umeme katika kijiji cha Nziga Kibaoni Tarafa ya Njinjo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini.
Aidha ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa namna ambavyo imeendelea kubadili vijiji kufanana na miji na pia kuweza kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kuwepo kwa kupitia nishati safi na salama.
Ndulane ameyasema hayo alipokuwa akiwasha umeme na kugawa mitungi ya gesi katika kijiji cha Nzinga Kibaoni.
Hatuna hiyo inakwenda pamoja na kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwaasa wananchi nchini kuhama katika matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mitungi hiyo ya gesi imegawiwa kwa wananchi kijijini hapo na Serikali kwa wajasiriiamali, vijana na wanawake kupitia REA.
Akielezea madhara yapatikanayo kwa matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa mifumo ya kiikolojia, magonjwa ya macho na mfumo wa kupumua.
Aidha amesema madhara mengine ni pamoja na ukatili wa kijinsia na wananchi kukosa muda wa kushiriki shughuli za kijamii, kiuchumi na kimasomo.
Amewataka wananchi wa kijiji cha nzinga kuchamkia fursa hii ya kuhama katika nishati isiyo salama na kujikita katika nishati safi ni rahisi kutumia ili kuokoa muda.
Pamoja na mambo mengine amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani alidhamiria kuhakikisha kuwa huduma ya nishati hususani umeme inapatikana kila mahali nchini.
Amewaomba wananchi kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuleta maendeleo nchini ikiwemo mawasiliano, maji na umeme pamoja na elimu.
Amewataka wananchi katika Kijiji cha Nzinga kuchamkia fursa ya umeme wa uhakika ambapo fursa nyingi za kiuchumi zitapatikana na umeme usitumike kuwasha taa tu bali utumike katika kuhakikisha unabadili maisha ya wananchi kwa kufungua mashine za kusaga na shughuli nyinginezo za kiuchumi
Kuhusu mradi wa REA mzunguko wa pili katika Jimbo la Kilwa Kaskazini amesema mradi ulikuwa na vijiji 16 lakini mpaka leo hii vijiji saba tayari vina umeme na vijiji vingine tisa vitaunganishwa kabla ya Novemba 30 mwaka huu.
Nzinga ni kijiji kikubwa kuliko vyote katika Jimbo la Kilwa Kaskazini kina idadi ya watu 9,500 kwa mujibu ya sensa ya mwaka juzi kupatikana kwa huduma ya umeme katika kijiji hiki kitasukuma maendeleo katika vijiji vingine na jimbo zima Kilwa Kaskazini.
‘’Namshukuru Mkurugenzi Mkuu REA kwa kuweza kutekeleza miradi yenye tija na inayoleta matunda katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini na Wilaya nzima ya Kilwa na kuwataka REA kuhakikisha wanakamilisha miradi yote ya mzunguko wa pili ikiwemo miradi ya vitongoji kumi na tano ‘’ Amesema Ndulane.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini REA, Hassan Saidy amesema Kijiji cha Zinga ni moja ya kijiji kinachopata umeme kupitia Wakala huo lakini pia ndani ya Jimbo la Kilwa Kaskazini kwa mwaka huu vitongoji 15 vitapatiwa umeme.
Amemshukuru Rais kwa kuipatia fedha za kutosha REA ili kuweza kutekeleza miradi hiyo.
‘’Nishati safi ya kupikia ni nyenzo muhimu kwani Mheshimiwa Rais ni muasisisi Barani Afrika na Tanzania ambapo ametoa maagizo kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wanahama kutoka katika matumizi ya nishati isiyo salama ya kupikia na kuhamia katika nishati safi ya kupikia,” amesema.
Amesema jiko la gesi na mtungi unaouzwa kwa kiasi cha sh 45,000 wananchi vijijini watanunua kwa bei ya sh 20,000 huu ni mkakati mahsusi ambapo Serikali kupitia REA italipia kiasi kilichobaki.
Amesema REA, itagawa takribani mitungi 450,000 nchi nzima na Wilaya ya Kilwa itapata takribani mitungi 3500 na itagawiwa sawa kwa majimbo ya Kilwa Kaskazini na Kilwa Kusini.
Kadhalika amesema serikali kupitia REA imegawa kiasi cha mitungi 231 katika vijiji vya Ndete Tarafa ya Kipatimo na kijiji cha Zinga Kibaoni Tarafa ya Njinjo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini