Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAIMU Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Flora Magige amesema mashindano ya walimu wanaofundisha lugha ya Kichina ni ushahidi wa dhati wa dhamira ya Taasisi ya Confucius kuimarisha ufundishaji wa lugha hiyo nchini.
Amesema hayo katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa walimu walioshiriki mashindano hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Confucius chuoni hapo, Profesa Magige amesema mashindano hayo ni jukwaa la kuonesha umahiri wa walimu wa Kichina kutoka Tanzania na China.

“Ushiriki wenu ni ishara ya ujuzi mkubwa mlionao katika lugha ya Kichina. Ni furaha kuona Taasisi ya Confucius ikiendeleza juhudi hizi za kutambua mchango wa walimu wake,” amesema.
Amesema Mashindano hayo yalihusisha walimu kutoka Taasisi ya Confucius ya UDSM na matawi yake, pamoja na washiriki kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Shule ya Sekondari Musabe ya Mwanza. Jumla ya walimu 27 wameshiriki mashindano hayo, wakiwemo walimu 18 kutoka China na tisa Watanzania.
Kwamba, Washiriki waligawanywa katika makundi mawili walimu Wachina na walimu Watanzania ambapo kila kundi lilitoa washindi watatu bora.

Aidha, walimu wanne wa ziada walipata zawadi za motisha kutokana na alama zao nzuri, na kufanya jumla ya washindi kufikia 10.
“Kwa wale ambao hawajashinda, wasikate tamaa. Ushiriki pekee ni ushindi,” amesema.
Kwa upande wao, Wakurugenzi wa Taasisi ya Confucius, Profesa Xiaozhen Zhang (Mchina) na Dkt. Mussa Hans (Mtanzania) wamesema walimu ni rasilimali muhimu katika kukuza lugha na utamaduni wa Kichina nchini Tanzania.

“Tunaamini kuwa mafanikio ya programu zetu yanategemea ubora wa walimu. Mashindano haya ni sehemu ya kutambua juhudi zao,” wamesema.
Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilianzishwa mwaka 2013 kwa ushirikiano kati ya UDSM, Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal nchini China, na Makao Makuu ya Taasisi za Confucius. Lengo kuu ni kukuza ushirikiano wa kielimu kati ya Tanzania na China, pamoja na kueneza maarifa ya lugha na utamaduni wa Kichina.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwambata wa Utamaduni wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Che Zhaoguang, amesema juhudi za kufundisha lugha ya Kichina zimepata msukumo mkubwa kutokana na kuimarika kwa uhusiano kati ya Tanzania na China.

“Lugha ya Kichina ni nyenzo muhimu katika kuimarisha mawasiliano, biashara, na uelewa wa kitamaduni kati ya mataifa yetu mawili. Tunafurahi kuona maendeleo haya,” amesema Zhaoguang.
Ameongeza kuwa taasisi na programu za lugha ya Kichina zimeongezeka nchini, zikiwemo UDSM, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro (MUM), na shule mbalimbali za sekondari.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika ubora wa walimu kupitia mafunzo na warsha endelevu.

“Tunatarajia kuona walimu wengi zaidi wakijiunga na programu za mafunzo ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza maarifa yao na kuendelea kukuza taaluma yao,” amesema.
Naye Mshindi wa kwanza ambaye ni Mhadhiri Msaidizi anayefundisha lugha ya kichina chuoni hapo, Emmanuel Legonga amesema amejisikia mwenye heshima na furaha kubwa kupokea tuzo hiyo kama mshindi wa mashindano hayo nchini.

“Ushindi huu si wangu pekee yangu ni wa wanafunzi wangu wote waliokuwa na imani nami, wa walimu walionilea, na wenzangu walionipa moyo na motisha,” amesema.
Amesema kufundisha kichina Tanzania ni zaidi ya kazi ni daraja la kuunganisha tamaduni mbili adhimu.

“Kila herufi tunayofundisha ni mbegu ya maelewano, urafiki na ushirikiano kati ya China na Tanzania,” amesema na kuongeza kuwa tuzo hiyo anaiweka mikononi mwa walimu wakichina wanaojitolea kila siku kwa bidii na moyo wa kujenga kesho iliyo bora zaidi,



