Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KITUO cha Afya Kimara kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam, kimekabidhiwa vifaa tiba vyenye thamani ya sh. Milioni 91 kwa watoto wachanga baada ya ujenzi wa ghorofa ya pili kukamilika.
Aidha kufanya jumla ya misaada yote iliyotolewa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kituo hicho kufikia Sh. Milioni 688.
Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dkt. Malamla Chaulenzi amesema hayo, wakati akitoa taarifa fupi ya kituo hicho leo Januari 27, 2025.

Chaulenzi amesema ghorofa hiyo ya pili inazinduliwa rasmi leo baada ya vifaa vyote kukamilika kwa msaada wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
“Ukamilifu wa ghorofa ya pili umesaidia sana kutatua tatizo la ufinyu wa eneo la kituo kwa sehemu kubwa na kutoa nafasi ya huduma za matibabu ya watoto na kliniki za kibingwa kufanyika na kuanzisha wodi ya watoto wachanga ambayo siku ya leo inazinduliwa rasmi,” amesema.
Amekiri kuwa kuwepo kwa wodi hiyo ya watoto wachanga kutarahisisha matibabu ya watoto wachanga hasa ikizingatiwa kituo hicho kinazalisha idadi kubwa ya watoto.
“Pia itaokoa gharama na usumbufu wa kwenda mbali kufuata huduma za afya katika vituo vingine,” amesema.
Amesema kanisa hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, walisaidia uboreshaji wa miundombinu kwa kujenga ngazi ya kupandia iliyogharimu zaidi ya Shilingi milioni 100.
Pia walianza ujenzi wa ghorofa ya pili wenye thamani ya Sh. Milioni 495.
Rais wa Kanisa hilo, Juventenious Rubona amesema mpaka sasa miradi iliyokamilika katika halmashauri hiyo imegharimu sh. Milioni 753.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni Shule ya Msingi Kibamba iliyofanyiwa ukarabati, Kituo cha Afya Kimara na Kituo cha Afya Makuburi.
Amesema miradi inayokaribia kukamilika kuwa imegharimu Sh. Milioni 522, pamoja na shule zilizoanza kukarabatiwa zinagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 1.1.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Ubungo, Dkt. Tulitweni Mwinuka ameshukuru kwa msaada huo na kuahidi kusimamia matumizi yake visiharibiwe.