Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAUMINI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wamehimizwa kulipa kodi ili kuiwezesha nchi kupata maendeleo.
Askofu Mkuu wa KKKT Dkt. Alex Malasusa amehimiza hilo wakati Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Juma Mwenda alipokwenda ofisini kwake kumsalimia.
Dkt. Malasusa amesema kwa kulipa kodi serikali itaweza kukamilisha malengo endelevu kwa munufaa ya watu wake.
“Hakuna nchi inayoendelea bila kodi. Ukiona Maendeleo ya nchi maisha bora ni sababu ya kodi wala hakuna muujiza hapo.
“Shida tunayopata ni wanaotoa kodi ni wachache hivyo mzigo unakuwa mkubwa, unawaelemea hao wachache walio waaminifu.
“Ili nchi iendelee lazima kuhakikisha binadamu anapata mahitaji muhimu ikuwemo chakula,” amesema.
Malasusa ameahidi kutoa elimu kanisani ili waumini waelewe na kıtımıza wajibu wao kama ilivyo kwenye maandiko matakatifu.
“Naahidi kushirikiana nanyi (TRA) kutoa elimu, kuwakumbusha kila siku pia kuwaambia kuwa maandiko yako wazi na tuheshimu mamlaka.
“Sasa tutashirikiana na wachungaji tuzungumzie ndani ya kanisa maana suala la kodi liliachwa sana tukawa tunahamasisha masuala mengine kama ya afya na mengineyo.
“Sasa tunafungua milango ya kuelezea hili ‘damu ya Tanzania’(kodi). Kanisa na taasisi zake zote watakuwa mstari wa mbele,” amesema.
Amesema elimu ya mlipa kodi ikipenyezwa makanisani watanzania watalipa kodi bila kulazimishwa na kwa furaha.
Awali Kamishna Mwenda amesema amefika ofisini kwa Askofu Malasusa kuona namna gani ya kushirikiana ili kuweza kutoa elimu kwa mlipa kodi.
“Kwa kuwa kanisa lina waumini wengi na hao ndio walipa kodi ni vizuri wajue kodi ipi inalipwa na ni kwa wakati gani na analipa wapi,” amesema.
Amesema kwa nafasi na fursa aliyonayo askofu ni rahisi kuwabadilisha waumini wake.
Amemshukuru Malsusa kwa utayari wake wa kukubali kushirikiana na TRA kuelimisha jamii.