Na Mwandishi Wetu
UBORESHAJI wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Geita na Kagera utafanyika kwa siku saba kuanzia Agosti tano hadi 11, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele amesema hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Geita leo.
Mkutano kama huo mkoani Kagera umefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa Mstaafu, Mbarouk Salim Mbarouk ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo.
“Mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mkoa huu wa Geita na Kagera ambapo uboreshaji utaanza Agosti tano hadi 11, mwaka huu ” amesema Mwambegele.
Maelezo yake ni kwamba, mikoa hiyo inafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa pili baada ya mzunguko wa kwanza ambao umejumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora ambako ulianza Julai 20, unatarajiwa kukamilika Julai 26 2024.
“Tume tayari imeanza uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma Julai 20 mwaka huu.
“Uzinduzi huo umeenda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi, utaendelea hadi Julai 26,” amesema.
Mkoani Kagera Jaji Mbarouk amesisitiza kadi za wapiga kura zilizotolewa 2015 na 2020, zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo.
Naye Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo, Kailima Ramadhan amesisitiza kuwa
wapiga kura wanaoboresha taarifa zao wanaweza kuanza mchakato wa awali kwa kutumia simu janja, kiswaswadu na kompyuta kupitia mfumo ujulikanao kama Online Voters Registration System (OVRS) au kwa kubobya *152*00#, kisha namba 9 na kufuata maelekezo.