Na Lucy Ngowi
ARUSHA: SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limezindua jengo lake jipya la biashara jijini Arusha, katika hafla iliyoambatana na utoaji wa vyeti kwa vyama wanachama wake, ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa mshikamano na upanuzi wa ushirikiano ndani ya shirikisho hilo.
Miongoni mwa vyama 16 vilivyotunukiwa vyeti ni Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA). Cheti hicho kilikabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, kwa Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, amesema kujiunga kwa JOWUTA kunafanya idadi ya vyama ndani ya TUCTA kufikia 16, kutoka 13 vilivyokuwepo awali.
Ametoa wito kwa waandishi wa habari kujiunga na JOWUTA ili kufurahia fursa mbalimbali, ikiwemo kutetewa kwa maslahi yao na kupewa elimu kuhusu haki na wajibu kazini.

Mbali na JOWUTA, vyama vipya vilivyopokea vyeti ni Chama cha Wafanyakazi Sekta ya Ulinzi Binafsi (TUPSE) na Chama cha Wafanyakazi wa Huduma za Viwandani Tanzania (TASIWU).
Kwa upande wake, Mussa Juma, Mwenyekiti wa JOWUTA, ameshukuru TUCTA kwa kutambua mchango wao na kuwapokea rasmi.
Amesema jukumu kubwa walilonalo sasa ni kuhakikisha wanahabari wanatetea maslahi yao na kufanya kazi katika mazingira bora.

“Tutaendelea kushirikiana na TUCTA kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria, wakiwa na mikataba rasmi na ajira zinazotambulika kisheria,” amesena.
Akihutubia katika uzinduzi huo, Waziri Ridhiwani amesema TUCTA lina mchango mkubwa katika historia ya nchi kabla na baada ya uhuru, na kwamba mafanikio mengi ya taifa hayawezi kutajwa bila kuwahusisha wafanyakazi.
“Asiyeona umuhimu wa shirikisho hili si mzalendo wa kweli. Serikali haitasahau wala kuwadharau wafanyakazi, kwani wao ndio chimbuko la mafanikio mengi ikiwemo elimu, miundombinu na huduma mbalimbali,” amesema Waziri Ridhiwani.