Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: UGONJWA wa fungashada ya migomba unasababishwa na virusi viitwavyo kitaalam virusi fungashada.
Huenezwa na wadudu wajulikanao kama vidukari wa migomba wanaopatikana katika eneo la shingo ya mgomba.
Kwamba wadudu hao husambaza ugonjwa maeneo ya ndani ya shamba.
Vile vile ugonjwa huo hauna tiba ya kikemikali, huathiri migomba ya aina zote.
Mtafiti kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), Fatma Mussa akielezea historia ya ugonjwa huo, anasema kwa mara ya kwanza ulionekana Tanzania katika mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Buhingwe mwaka 2020.
Baada ya kuonekana huko, anasema hivi sasa ugonjwa huo umesambaa katika mikoa mbalimbali ukiwemo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mbeya, Dodoma, Kilimanjaro na Mwanza.
Fatma akielezea athari za ugonjwa huo anasema unaweza kusababisha hasara kati ya asilimia 90 hadi 100 ya uzalishaji wa ndizi ndani ya msimu mmoja baada ya shamba kuambukizwa.
“Mkulima atapata hasara katika kipato kitokanacho nau uzaji wa ndizi. Familia na jamii zitapoteza vyanzo vya chakula cha asili, aina ya migomba inayopendwa na wakulima inaweza kupotea,
“Na shamba likishambuliwa litagharimu fedha nyingi kulirudisha katika hali ya uzalishaji wa ndizi, kwa kulipia gharama za usafishaji shamba kwa kutoa migomba yote na kuweka mazao mengine kwa muda ili kuhakikisha vidukari vinatokomea kabla ya kuweka migomba mipya shambani,” anasema.
Fatma anataja dalili za ugonjwa huo kuwa ni udumavu mkali wa mgomba, pia mgomba ulioathirika kwa muda mrefu majani yake hufungamana na kuonekana kama shada la maua.
“Vile vile majani ya mgomba huchongoka mithili ya mkuki, mistari ya kijana kwenye ubavu wa kati wa jani karibu na shingo ya mimea, majani kuwa magumu, yanakuwa njano na baadaye kukauka,” anasema.
Anaongeza kwamba, migomba iliyoathirika na ugonjwa kabla ya kuanza kwa maua haiwezi kuzaa kabisa, wakati mimea iliyoathiriwa baada ya hatua ya kutoa maua kiwango cha uzalishaji kitapungua kati ya asilimia 90 hadi 100.
Kuhusu kuenea kwa ugonjwa huo anasema virusi vya fungashada ya migomba huenezwa na wadudu hao vidukari wanaobeba ugonjwa kutoka katika mmea ulioathirika kwenda kwa mmea wenye afya.
Kwamba vidukari hao huishi kwenye kingo za majani ya mgomba eneo la shingo ya mmea wakifyonza chakula chao toka kwenye mgomba.
“Vidukari hueneza ugonjwa ndani ya shamba na maeneo ya karibu. Jina la kitaalaam la vidukari ni Pentalonia Nigronervosa, lakini wakulima wa Tanzania wanawaita mdudu huyo Aphid au inzi wa mafuta,” anasema.
Anasema njia nyingine ya kuenea kwa ugonjwa ni kwa kuhamisha vipando vilivyoathirika kutoka eneo moja kwenda jingine, ambapo njia hiyo ndio hueneza ugonjwa kwa umbali mrefu ndani ya mkoa na nchi.
Anaelezea jinsi ya kudhibiti ugonjwa huo ni kuacha kutumia mbegu ambayo imeathiriwa na ugonjwa.
“Acha kusafirisha vipando kutoka eneo moja kwenda lingine bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kudhibiti afya ya mimea,” anasema.
Pia udhibiti mwingine anasema ni kutoa taarifa kwa Ofisa Ugani au uongozi wa Kijiji pale kunapokuwa na dalili za ugonjwa katika shama.
Mbinu nyingine za kitamaduni ni kukagua shamba mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kung’oa migomba iliyoathirika kuanzia kwenye mizizi.
“Kata kata migomba uliyoing’oa vipande vidogo vidogo kuepuka kuchipua tena, chama moto na fukia masalia.
“Kagua shamba mara kwa mara kuhakikisha hakuna machipukizi tena, na kama machipukizi yatatokea, tokomeza chipukizi jipya kwa dawa ya kiua gugu,” anasema.
Kwa mbinu za kisayansi anashauri mkulima kuchanganya lita moja ya kiua gugu na lita nne za maji kwenye chombo safi, kisha auchukue mchanganyiko huo kwa kutumia sindano kubwa yenye ujazo wa milimita 10 kisha achome migomba iliyoathirika, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dawa yote imeingia kwenye mgomba.
Fatma anasema, “Kwa migomba mikubwa choma dawa sehemu tatu kuanzia chini ya shina la mgomba, katikati na juu ya shinda.
“Kwa migomba ya saizi ya kati inashauriwa kuchoma dawa mara mbili , chini ya shina la mgomba na juu karibu na yanapochanua majani.
“Kwa migomba inayochipukia inashauriwa kuchoma dawa sehemu moja tu katikati ya shinda, Hakikisha sindano imezama yote ili kuhakikisha dawa imefika kwenye kiini cha migomba,” anasema.
Maelezo yake ni kwamba, baada ya hapo mkulima atasubiri kwa wiki mbili mpaka pale migomba itakapokufa ndipo ing’olewe kwenye shamba.
“Nji hii inapunguza kuendelea kuenea kwa ugonjwa kwa kuua migomba yote iliyoathirika,” anasema.
Anataja viua dudu vilivyopendekezwa kuwa ni Glyphosate 480 na Glyphosate 360.
Fatma anasema kwamba utafiti wa ugonjwa huo walianza kuufanya mwaka 2023.
Naye Ofisa Mawasiliano wa IITA, Gloriana Ndibalema anasema kwa sasa hivi Afrika Mashariki ina changamoto ya fungashaba ya migomba, hivyo wameshirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), na Mamlaka ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), pamoja na Taasisi inayoshughulika na Kilimo cha Mboga mboga na matunda nchini (TAHA).
Gloriana anasema ugonjwa huo umetokea hauna dawa lakini unaweza kudhibitiwa.
Anasema suluhu ya ugonjwa huo bado haijapatikana, watafiti bado wanapambana kutafuta suluhu.
Anasema katika kupata miche mipya watafiti wa nashauri kupata mbegu safi zinazozaa vizuri.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Maruku kilichopo Kagera, Dkt. Mpoki Shemwela anaelezea ushirikiano uliopo kati ya taasisi hiyo na IITA.
Anasema muda mrefu taasisi hiyo ya kilimo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na IITA, ushirikiano ambao umekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha uzalishaji wa kilimo kupitia uboreshaji wa mazao, mifumo ya mbegu, na udhibiti wa wadudu na magonjwa.
Anasema kwamba, ushirikiano huo pia upo kwenye kutatua changamoto za visumbufu vya mazao ambavyo ni wadudu na magonjwa.
“TARI kwa kushirikiana na IITA wamekabiliana na vitisho vikubwa kwa uzalishaji wa mazao, vikiwemo wadudu na magonjwa. Kwa mfano, wamefanya tafiti za ufuatiliaji wa Virusi vya Ugonjwa wa fungashada (BBTV) na kuandaa mafunzo kwa wakulima na maafisa ugani.
“Juhudi hizi zinalenga kujenga uwezo katika kugundua mapema, kuzuia, na kudhibiti BBTV, ili kulinda uzalishaji wa ndizi katika maeneo yaliyoathirika. Tangu ugonjwa huu ulivyo ripotiwa mwaka 2021, TARI na IITA wamfeanya kazi bega kwa bega katika kukabilina na ueneaji wa ugonjwa huu hatari,” anasema.
Dkt. Mpoki anasema kupitia ushirikiano unaoendelea, TARI na IITA wanaendelea kuendeleza ubunifu wa kilimo, kuboresha maisha ya watu, na kuimarisha usalama wa chakula Tanzania na kwingineko.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo Mkuu kutoka TPHPA, Hamad Lyimo anasema kwamba kama mamlaka inaosimamia afya ya mimea nchini, masuala yote yanayohusu afya ya mimea ikiwemo migomba wanayasimamia.
Anasema wanashirikiana na taasisi za kimataifa kubadilishana uzoefu, kushirikiana kwenye tafiti ikiwa ni pamoja na kupata suluhisho la tatizo linalokuwepo.
“Tunashirikiana hasa kwenye magonjwa ya kipaumbele ikiwepo ugonjwa wa fungashada ya migomba, mnyauko wa migomba, magonjwa kama sigatoka na mnyauko wa bakteria, ili kujua hali ikoje nchini,” anasema.