Na Lucy Ngowi
SHIRIKA la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), kwa kushirikiana na Baraza la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki (IUCEA) linaratibu programu ya mafunzo ya uchambuzi wa data kidijitali kwa vijana na wanafunzi mbalimbali waliomaliza vyuo.
Lengo likiwa ni kuwezesha kupata ujuzi wa kidijitali utakaosaidia kuwa wabobevu katika soko la ajira katika maeneo mbalimbali.
Mkuu wa program hiyo kutoka GIZ, David Roos amesema hayo katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ( DIT), katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa wanafunzi wa vyuo vikuu walionufaika na mafunzo hayo.
Maelezo yake ni kwamba, program hiyo ya mafunzo ni maalum inayowawezesha wahitimu wa vyuo vikuu wasio na ajira na mahitaji ya lazima kupata ujuzi wa uchambuzi wa data, taswira, na ustadi wa kutengeneza simulizi ili kuongeza uwezo wa kuajiriwa .
Amesema katika mafunzo hayo ya siku 10, wahitimu wamepata elimu ya muhimu ya data na ujuzi wa uchambuzi wa data, kuongezeka kwa uwezo wa kuajiriwa, na fursa za kazi kwa washiriki kote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki( EAC)
Amesema washiriki walichaguliwa kutoka kundi la wahitimu wa vyuo vikuu wasio na ajira kutoka katika nchi za Burundi, DRJamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, na Uganda.
.
“Kupitia mfululizo huu wa mafunzo, lengo letu ni kuimarisha uwezo wa kuajiriwa na hata kuwezesha vijana kukubalika katika soko la ajira,” amesema Roos na kuongeza kuwa tayari vijana 84 wamepatiwa mafunzo hayo katika nchi wanachama wa EAC.
Mshiriki wa mafunzo hayo Michael Chongeni ambaye ni mhitimu wa uhandisi kwenye Mafuta na gesi kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) amesema mafunzo hayo yanawezesha kuwa wachambuzi wazuri wa data na ambayo yanaongeza ujuzi.