Na Danson Kaijage
DODOMA: WANANCHI katika Jiji la Dodoma, wamejitokeza kwa wingi kumlaki Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais.

Tukio hilo limekuja baada ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kutangaza ratiba ya uchukuaji wa fomu kwa wagombea wa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, uchukuaji wa fomu kwa nafasi ya Urais umeanza Agosti tisa, na unatarajiwa kukamilika Agosti 27, 2025, huku fomu za Ubunge na Udiwani zikitolewa kuanzia Agosti 14 hadi Agosti 27, 2025.
Samia Suluhu Hassan amekuwa mgombea wa kwanza kuchukua fomu ya Urais kupitia chama chake, CCM, akifuatana na mgombea mwenza wake, Dk. Nchimbi.

Shangwe na nderemo vilitawala maeneo mbalimbali ya Dodoma, hasa katika jengo la Makao Makuu ya CCM, ambako mamia ya wananchi walikusanyika kushuhudia tukio hilo. Wasanii maarufu akiwemo Dulla Makabila na vikundi mbalimbali vya burudani walikuwepo kusherehesha mapokezi hayo, hali iliyozidisha hamasa ya tukio hilo la kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amesema zoezi la uchukuaji wa fomu kwa wagombea wa Urais lilianza rasmi saa 4:50 asubuhi, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na tume hiyo.

